Friday, February 1, 2019

DC KAWAWA ATOA SALAMU ZA SERIKALI CHALINZE

Image may contain: 1 person, sitting and indoor
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mheshimiwa Zainabu Kawawa akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani Halmashauri ya Chalinze.
................................. 


Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mheshimiwa Zainabu Kawawa amewataka waheshimiwa madiwani wa Halmashauri  ya Chalinze wilayani humo, kuwaelimisha wafanyabiashara wadogo ili wapate vitambulisho vya ujasiriamali ambavyo vimetolewa na serikali kwa kulipia Tsh 20,000.


Aidha amewaonya wanasiasa kutoingiza siasa katika zoezi la ugawaji vitambulisho bali zoezi hilo lizingatiwe sheria taratibu na miongozo iliyotolewa na serikali katika kuwakwamua wajasiriamali kiuchumi,na akaagiza zoezi hili liwe limekamilika kabla ya mwezi Machi mwaka huu.


Mheshimiwa Kawawa akazungumzia ufaulu wa matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2018 na kuipongeza Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo kwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa na kuitaka Halmashauri  ya Chalinze kuweka mikakati ya ushindi kitaaluma kama ilivyo kwa Halmashauri ya Bagamoyo. 


Hata hivyo Mheshimiwa Kawawa aligusia changamoto ya ukosefu wa maji katika Halmashauri ya chalinze na kulaani kitendo cha mkandarasi aliyeahidi kupatikana kwa maji wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuendelea kulifanyia kazi suala la maji.


Mwisho Mama Kawawa aliwashukuru watendaji wa Halmashauri ya Chalinze kwa kumpa ushirikiano katika utendaji kazi na kuwataka wataalamu wafanye kazi zao kwa kuzingatia taaluma zao na kuwa wakweli kwa utekelezaji wa Majukumu ya serikali "Nataka serikali inapotoa fedha za miradi nione mradi umetekelezeka kwa wakati pasipo ubabaishaji hiyo ndiyo kazi ya mwanasiasa kuona matokeo".Kawawa alisema.


Imeandaliwa na msemaji wa Halmashauri ya Chalinze.
Image may contain: 4 people
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa alipokuwa akizungumza katika kikao hicho.


No comments:

Post a Comment