WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku 16 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Rombo, Magreth John awe amepeleka asilimia 20 sawa na sh milioni 114 ya kijiji
cha Holili kabla ya Machi 10 mwaka huu, fedha hizo zinatokana na mauzo ya
madini ya pozolana.
Ametoa
maagizo hayo leo (Jumamosi, Februari 23, 2019) wakati akizungumza na watumishi
wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Holili pamoja na wananchi wa kijiji cha Holili,
akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro.
Kituo hicho kipo katika
mpaka wa Tanzania na Kenya.
Waziri
Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya wananchi wa kijiji cha Holili kuwasilisha
malalamiko yao kupitia mabango wakimuomba awasaidie ili Halmashauri hiyo iweze
kulipa fedha zao zinazotokana na mapato ya mauzo ya madini hayo yanayochimbwa
kijijini kwao.
“Mkuu
wa wilaya (Agness Hokororo) simamia kuhakikisha kiasi hicho cha fedha
kinakwenda kwa wananchi na Mkuu wa Mkoa (Dkt. Anna Mgwira) nataka nipate
taarifa kuwa fedha hizo zimeshalipwa kwa uongozi wa kijiji husika.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka watendaji katika maeneo mbalimbali nchini kuwa
wamepelekwa huko kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo hawana budi kutenga
muda wa siku tatu kwa wiki na kwenda maeneo ya vijijini kusikiliza kero
zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amesema hali ulinzi na usalama katika mpaka huo si nzuri,
Serikali imeamua kuimarisha ulinzi kwenye mpaka huo, hivyo ni muhimu kwa
wananchi washirikiane katika kuulinda mpaka huo.
Hivyo,
Waziri Mkuu ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata na kuwachukulia
hatua watu wote watakaokamatwa wakipita au kuingiza mizigo kupitia njia zisizo
rasmi kwa sababu hao ndio wanaopitisha silaha.
Waziri
Mkuu amesema wananchi wa Tanzania na Kenya hawajazuiwa kufanya biashara upande
wowote bali wanatakiwa wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika nchi
husika ikiwa ni pamoja na kutumia njia rasmi.
Amewataka
viongozi na watendaji waliopo maeneo ya mipaka huo wa Holili wawe makini kwa
sababu mpaka huo hauko salama na kuna mambo mengi yanayoendelea ambayo yapo
kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment