Baraza la
Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Chalinze limekaa na kupitisha bajeti ya
Mapato na matumizi ya jumla ya Fedha za kitanzania bilioni 50.6 kwa mwaka wa
Fedha 2019/2020.Mapendekezo ya bajeti hiyo yamefanyika katika kikao maalumu cha
baraza hilo kilichofanyika katika Ukumbi wa shule ya Sekondari ya Lugoba jana.
Akiwasilisha
bajeti hiyo Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Bwana Shabani
Millao alitoa ufafanuzi wa bajeti na kueleza mawanda ya bajeti(scopes of
budget)hiyo kuwa,Mapato ya ndani bilioni 6.1,michango ya Jamii bilioni 1.8,ada
za shule za Sekondari milioni 84.6,mishahara bilioni 31.7,miradi ya maendeleo
serikali kuu bilioni 5.8,ruzuku ya matumizi ya kawaida bilioni 3.9,wahisani
bilioni 1.2.
Hivyo kutokana na ufafanuzi huo bajeti ya halmashauri ya Wilaya ya
Chalinze inakuwa na bajeti yenye jumla ya Fedha za kitanzania bilioni 50.6.
Katika
mapendekezo ya bajeti baraza la Madiwani lilipitia kwa kina kamati kwa kamati
na kuona vipaumbele ambavyo vinatatua kero za wananchi kama huduma za
afya,elimu Maji na usafi wa mazingira na wajumbe walishauri baadhi miradi
iondolewe kwa sasa ili huduma za Jamii zitolewe moja kwa moja,katika mabadiliko
ya miradi waliyopendekeza wajumbe ni kuondoa mradi wa ujenzi wa nyumba za wakuu
wa idara na kukamilisha vituo vya afya ,zahanati na vyumba vya madarasa ambavyo
ni kipaumbele kwa sasa.
Naye Diwani wa viti maalum CCM Maria Moreto aliwaomba Madiwani kumuunga mkono hoja ya kuondoa mradi wa ujenzi wa nyumba za wakuu wa idara kwa sasa ili kukamilisha miradi ya wananchi na wananchi waanze kupata huduma, mradi wa ujenzi wa nyumba za wakuu wa idara ufanyike bajeti ijayo.
Mwenyekiti Wa halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mhe Saidi Zikatimu alitoa mchango wake wa mawazo kwa kueleza umuhimu wa miradi katika halmashauri na kuwataka wajumbe kuamua kwa kuzingatia miongozo ya bajeti na si vinginevyo kwani tunapanga bajeti kwa miongozo iliyotolewa na serikali.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Miono ambaye pia ni makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mheshimwa Juma Mpwimbwi aliwapongeza wataalamu kwa maandalizi mazuri ya bajeti na kwa ufafanuzi mzuri wa mawanda ya bajeti Iliyofafanuliwa na Kaimu Mkurugenzi, "Ni bajeti inayogusa Maisha ya wananchi na inayotatua kero za wananchi katika halmashauri yetu,bajeti hii itatekelezeka kama tutakusanya Mapato yetu kwa umakini na kufikia malengo tuliyojiwekea." Mpwimbwi alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Bwana Shabani Millao aliwashukuru wajumbe wa baraza la Madiwani kwa kupitia kwa kina bajeti pendekezwa na kueleza kuwa bajeti hii imeandaliwa kwa kuzingatia miongozo ya serikali na kila kinachosomeka ni kipaumbele kwani mwongozo ndiyo uliotumika katika kuandaa kazi hii. "Ushauri mlioutoa ni wa kujenga na pale itakapowezekana kulingana na ukomo wa bajeti tutatekeleza na ikishindikana kwa mwaka huu tutatekeleza kwa bajeti ijayo“ Millao alisema.
Hata hivyo baada ya mjadala wa muda mrefu kwa pamoja Madiwani waliridhia kupitisha bajeti ya halmashauri yenye thamani ya Fedha za kitanzania bilioni 50.6.
No comments:
Post a Comment