Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst)
George Mkuchika (Mb), akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ruangwa mkoani Lindi (hawapo pichani) katika kikao kazi kilichofanyika katika
ukumbi wa halmashauri hiyo. Kushoto ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Dkt.
Bora Haule.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst)
George Mkuchika (Mb), akijibu hoja za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ruangwa mkoani Lindi (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika
katika ukumbi wa halmashauri hiyo. Kushoto ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa
Lindi, Dkt. Bora Haule.
..................................
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George
H. Mkuchika amewakumbusha Maafisa Utumishi kuingiza taarifa sahihi za watumishi
kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ili
kutozalisha watumishi hewa na kupunguza kero kwa wastaafu katika kupata haki
zao kama inavyostahili.
Mhe. Mkuchika ameyasema hayo wilayani
Ruangwa wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa
mkoani Lindi, kabla ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, endapo
maafisa utumishi watashindwa kuingiza taarifa sahihi za watumishi kwenye mfumo
wa HCMIS itasababisha kupoteza taarifa na ikitokea mtumishi kufariki au
kustaafu itapelekea Ofisi ya Rais Utumishi kukosa taarifa sahihi za mtumishi
huyo wanapotaka kuandaa stahili zake.
“Niwakumbushe maafisa utumishi nchini
kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu kwa kuwahudumia ipasavyo watumishi wa umma
walio katika maeneo yenu ya kazi na wananchi kwa kutoa huduma bora kwa wakati
na bila upendeleo,” Mhe. Mkuchika amesema.
Aidha, Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa,
endapo maafisa utumishi watatekeleza wajibu wao ipasavyo, watumishi wastaafu
watapata haki yao ya kulipwa mafao kwa wakati kama inavyostahili na kuwahimiza
maafisa utumishi kufuatilia mafao ya watumishi wastaafu kwa moyo bila
kulazimishwa wala kutaka rushwa.
Mhe. Mkuchika amesema kuwa, ili
Serikali iweze kufanikisha zoezi la ulipaji mafao kwa mtumishi mstaafu kwa
wakati na kwa usahihi, ni wajibu wa Afisa Utumishi kuhakikisha taarifa zilizopo
kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ni
sahihi.
“Si jambo zuri kwa mtumishi kusafiri
kutoka kituo chake cha kazi kwenda Ofisi ya Rais Utumishi, Dodoma kufuata
huduma ambayo Afisa Utumishi anaweza kuitatua,” Mhe. Mkuchika amesisitiza.
Mhe. Mkuchika ameweka bayana kuwa,
endapo mtumishi atafuata huduma Ofisi ya Rais Utumishi, atamrudisha mtumishi
huyo kwenye kituo chake cha kazi ili jambo lake lifanyiwe kazi na Afisa
Utumishi husika.
Ameongeza kuwa, Serikali imetoa
mafunzo ya matumizi ya mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara
(HCMIS) kwa maafisa utumishi lakini mpaka sasa, Ofisi ya Rais Utumishi imekuwa
ikipokea malalamiko ya watumishi wanaosafiri kutoka vituo vyao vya kazi kwenda
Dodoma kuangalia taarifa zao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H.
Mkuchika (Mb) yuko katika ziara ya kikazi mkoani Lindi yenye lengo la kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF mkoani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hashim Mgandilwa akitambulisha makundi ya watumishi waliohudhuria kikao kazi kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo mkoani Lindi.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ruangwa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) (hayupo
pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya
wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Katibu wa Chama cha Walimu
wilaya ya Ruangwa, Bi. Suzan Eliamini akiuliza swali wakati wa kikao kazi kati
ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) na watumishi wa halmashauri
ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri
hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akikagua ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Namkonjela, wilayani Ruangwa mkoani Lindi iliyojengwa kwa fedha za TASAF. Kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Mahela Godfrey na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Dkt. Bora Haule.
No comments:
Post a Comment