Wednesday, February 27, 2019

KATIBU MKUU NISHATI ASIFU WATAALAMU TANESCO


KATIBU Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua,(watatu kulia), akizungumza na vyombo vya habari mbele ya mashine (turbine) ya kufua umeme inayofanyiwa matengenezo makubwa ya kujilinda kwenye kituo cha kufua umeme wa gesi asilia cha Ubungo II, jijini Dar es Salaam.

KATIBU Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, amewapongeza wataalamu wa Shirika la Umeme Nchini TANESCO kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhakikisha umeme unawafikia wateja licha ya changamoto ambazo zinawakabili

.

Dkt. Mwinyimvua ametoa pongezi hizo leo Februari 26, 2019 wakati alipotembelea vituo vya kufua umeme wa gesi  vya Ubungo I, Ubungo II, Songas lakini pia kuona kazi ya kufunga transfoma mpya kwenye kituo kikuu cha kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo.  Dkt. Mwinyimvua ambaye alifuatana na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, amesema “Tunazitambua changamoto zinazowakabili, lakini niwapongeze kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wateja.” Alisema.

Akitoa taarifa ya Kituo cha kufua umeme utokanao na gesi asilia cha Ubungo II, Meneja wa kituo Mhandisi Lucas Busunge, alisema kituo hicho kina mashine tatu za kufua umeme kila moja ikizalisha Megawati 43 na hivyo kufanya jumla ya Megwati 129.

Adha kwa sasa kituo hicho kiko kwenye matengenezo makubwa ya kinga yaani (Preventive maintanence), kwa jina la kitaalamu matengenezo hayo huitwa Level C Inspection na hufanyika baada ya mitambo kutembea zaidi ya masaa 40,000 tangu kituo kianze kuzalisha umeme, alisema Mhandisi Busunge.

“Matengenezo haya yatahusisha mitambo yote mitatu na mtambo wa kwanza ulianza kutengenezwa Januari 9, 2019 katika mtambo namba mbili na yatafanyika kwa awamu kwa kuzima mtambo mmoja baada ya mwingine hadi yatakapokamilika na tunatarajia kazi hii ya kufanya matengenezo itakamilika Juni 5, 2019.” Alifafanua.

Matengenezo  hayo yanaambatana na marekebisho ya kufanya mitambo isizime kwa masaa 40 kila baada ya umeme wa Gridi ya Taifa kukatika kama ilivyo hivi sasa ambapo Gridi ya Taifa ikitoka basi mitambo ina block kwa masaa 40 kabla ya kurejea katika hali yake ya kawaida.

“Marekebisho hayo yataiwezesha mitambo kuweza kuanzisha Gridi kama ilivyo katika vituo vya Kidatu kuweza kurejesha umeme kwa haraka. Hivyo marekebisho haya yatawezesha mitambo kurejesha umeme kwa haraka jijini Dar es Salaam wakati umeme wa Gridi ya Taifa unapokatika.” Alibainisha Mhandisi Busunge.

Katika siku za hivi karibuni kunekuwepo na changamoto ya upatikanaji umeme kwa wakati wote baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam ambapo imeelezwa kuwa sehemu kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani hutegemea Kituo Kikuu cha kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo ambacho kina transfoma mbili kubwa kila moja ina uwezo wa kusukuma Megawati 110 kila moja na kufanya jumla ya Megawati 220, lakini pia kuna Megawati zingine 300 kutoka vyanzo vingine vya Songas, Ubungo II na Tegeta na kufanya jumla ya Megawati 520 wakati mahitaji halisi ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani ni Megawati 570 na hapo kunakuwa na upungufu wa Megawati 50.

Kutokana na upungufu huo, Serikali kupitia Shirika la Umeme Nchini TANESCO imechukua hatua ya kununua Transfoma kubwa yenye uwezo wa kusukuma takribani Megawati 240 kutoka kwenye msongo wa kilovoti 220 kuelekea Msongo wa kilovoti 132 ili kuongezea nguvu umeme unaotumika katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani, ameongeza Meneja Miradi wa TANESCO Mhandisi Stephene Manda.

“Tunao umeme wa kutosha kilichokuwa kinasumbua ni namna ya kuushusha umeme huo wa msongo wa kilovoti 220 na kuushusha hadi msongo wa kilovolti 132 na ndiyo kazi tunayofanya hivi sasa ya kufunga transfoma mpya ambayo itatatua changamoto hiyo.” Alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Hamisi Mwinyimvua.

Pia Dkt. Mwinyimvua aliwapongeza TANESCO kwa ubunifu walioufanya wa kufanya marekebisho kwenye mitambo yake mitatu ya Kituo cha kufua umeme wa gesi asilia cha Ubungo II ambapo baada ya marekebisho hayo, umeme ukitoka kwenye Gridi ya Taifa, basi mitambo hiyo inaweza kuingilia kati na hivyo kulifanya jiji la Dar es Salaam na kuwa salama kwa maana ya kutoathirika kwa kutoka kwa Gridi ya Taifa.

 Dkt.Mwinyimvua (wapili kushoto), na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, (kulia), wakiongozwa na Meneja Miradi wa TANESCO, Mhandisi Stephene Manda, (kushoto), walipotembelea kuona transfoma hiyo.

 Hii ndiyo transfoma kubwa mpya yenye uwezo wa kusukuma umeme wa Megawati 240, ambayo inafungwa kwenye Kituo kikuu cha kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo na hivyo kufanya kituo hicho kuwa na transfoma tata.

 Wataalamu wakiwa kwenye chumba cha SCADA wakifuatilia mwenendo wa umeme kutoka vyanzo na vituo mbalimbali vya umeme nchini. Kituo hiki kiko Ungungo.



 Meneja wa Kituo cha kufua umeme utokanao na gesi asilia cha Ubungo II, Mhandisi Lucas Busunge, (kushoto), akifafanua jambo mbele ya Katibu Mkuu, Dkt. Mwinyimvua (wapili kulia) na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, (watatu kushoto).


Mhandisi wa TANESCO ambaye anahudumu kwenye chumba cha udhibiti (control room) cha kituo kikuu cha kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu na ujumbe wake, walipotembelea kituo hicho leo Februari 26, 2019.

No comments:

Post a Comment