NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA
KATIKA kukabiliana na changamoto ya utoaji wa huduma
ya afya kwa wananchi, serikali ya awamu ya tano inajenga hospitali za
wilaya tatu za kisasa , halmashauri ya Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini na Kibiti
mkoani Pwani ambazo zitagharimu kiasi cha sh. bilioni 4.5.
Akizungumza wakati alipotembelea ujenzi wa hospital ya
halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Lulanzi kata ya Pichandege, kwenye ziara yake
inayoendelea kukagua miradi ya maendeleo, mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi
Evarist Ndikilo alisema kukamilika kwa hospital hizo, kutaondoa kero ya
kutembea umbali mrefu kufuata matibabu.
“Kila hospital inatarajiwa kugharimu bilioni 1.5 ,matarajio
yetu ni kuona ujenzi unakamilika na sio kuanza mradi na kisha kusuasua
“alieleza Ndikilo.
Aidha ameelezea, fedha zote zinazoelekezwa katika miradi
hiyo muhimu zitumike kwa wakati na kwa matumizi lengwa bila kuziacha kubaki
viporo.
Hata hivyo Ndikilo, aliwaasa wahandisi wa halmashauri ya
Kibaha Mji na wa serikali ya mkoa huo kujiwekea utaratibu wa kutoka maofisi
kwenda kutembelea miradi pasipo kusubiria ziara ama kiongozi kutembelea ndipo
nao watoke maofisini.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama alitoa rai
kwa jamii kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili
sekta ya elimu na kujitolea kwenye miradi ya kimaendeleo.
Diwani wa kata ya Picha ya ndege Robert Machumbe
alieleza, nia ya serikali ni kuwaletea wananchi mabadiliko chanya
ya kimaendeleo ambapo amefafanua kwamba, eneo hilo linalojengwa hospital
lina ukubwa wa hekari 25 lipo eneo linalojengwa shule ya sekondari Lulanzi
lenye ukubwa wa hekari 11.7 .
No comments:
Post a Comment