Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Eng.
Evarist Ndikilo amefanya ziara maalum ya kutembelea, kukagua na kuhimiza
Wananchi kushiriki shughuli za maendeleo hususani kuchangia ujenzi wa madarasa
ya Shule za Sekondari.
Ziara hiyo ya siku moja iliyoanzia katika Kata ya Mapinga ambapo Mkuu wa Mkoa alipokelewa na Mwenyeji wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Zainab Kawawa, ilikua na lengo la kuhamasisha Wananchi kushiriki kikamilifu kuchangia ujenzi wa madarasa katika Shule za Sekondari za Kata, Wilayani Bagamoyo, ili wanafunzi waliochaguliwa awamu ya pili kujiunga na elimu ya Sekondari kuhakikishiwa nafasi ya kujiunga na elimu hiyo.
Akizungumza na Wananchi katika Mkutano maalum wa majumuisho ya Ziara hiyo uliofanyika katika Kijiji cha Kongo, kilichopo Kata ya Yombo Wilayani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Eng. Evarist Ndikilo amewaasa Wananchi kuacha kuisusia Serikali kujenga miundombinu ya elimu kwa kisingizio cha elimu bure.
Akifafanua Mhe. Eng. Ndikilo amesema kuwa dhana ya elimu bila malipo haimaanishi Wazazi kutochangia kabisa gharama za elimu, bali Serikali inampunguzia mzazi gharama hizo kwa kumlipia mwanafunzi ada, chakula kwa wanafunzi wa bweni pamoja na gharama zingine za uendeshaji wa Shule lakini ujenzi wa miundombinu kama madarasa na madawati ni wajibu wa kila Mwananchi kuchangia ili wanafunzi wapate mahala pa kujifunzia na pale Wananchi wanapofanya vizuri katika ujenzi wa miundombinu, basi Serikali huunga mkono juhudi hizo za Wananchi.
“Nawaagiza Wakuu wote wa Wilaya za Mkoa wa Pwani na Wakurugenzi wote wa Halmashauri wahakikishe Wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari wanapata nafasi hiyo, hususani wale waliochaguliwa awamu ya pili, fanyeni jitihada za makusudi kukamilisha vyumba vya madarasa vinavyoendelea kujengwa sasa ili Wanafunzi hao wapate nafasi ya kuendelea na elimu ya Sekondari” Amesema Ndikilo.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainab Kawawa akitoa takwimu za ufaulu wa kidato cha kwanza kiwilaya, amesema jumla ya Wanafunzi 1869 walichaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari kwa Mwaka 2019 katika awamu ya kwanza, na awamu ya pili jumla ya Wanafunzi 482 wamechaguliwa huku Wilaya ya Bagamoyo ikiwa na upungufu wa vyumba 32 vya madarasa hadi sasa.
Pamoja na uhamasishaji huo wa Wananchi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa, Mkuu wa Mkoa pia ametumia Ziara hiyo kukagua na kutembelea miradi ya maendeleo ya Sekta ya miundo mbinu ya barabara, Afya na shughuli za wanufaika wa TASAF, ambapo amekagua ujenzi wa mfereji wenye ukubwa wa mita 500, mradi uliotekelezwa na wakala wa barabara vijijini (TARURA) katika Kata ya Dunda, Ujenzi wa Kituo cha Afya Matimbwa, Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Mapinga katika Kata ya Mapinga na Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na Ofisi moja ya Walimu katika Shule ya Sekondari Hassanal Damji, iliyopo Kata ya Magomeni.
No comments:
Post a Comment