Tenki hili limekamilika katika Halmashauri ya
Kilindi na wananchi walianza kufurahia kupata maji. Matokeo yake Pampu
imeungua. Waziri wa Maji Mhe. Profesa Mbarawa amemuagiza Mkandarasi kuhakikisha
ananunua pampu mpya na kuifunga haraka iwezekanavyo na siyo kufanya
ubabaishaji.
Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Lushoto Bw.
Baraka Rajab akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 650,000
linaloendelea kujengwa eneo la Magamba
..............................
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb)
amewataka wananchi wa mkoa wa Tanga kwa ujumla kutunza vyanzo vya maji ili viwe
endelevu kwa kikazi chetu na kizazi kijacho. Pia amewata watunze miundombinu na
kulipa bili za maji kwa wakati.
Waziri Mbarawa aliyasema hayo alipokuwa akizunguka katika Halmashauri za Mkoa huo kukagua miradi ya maji inayotekelezwa katika Mkoa huo.
“Hakikisheni mnatunza vyanzo vya maji na kuvilinda, tusipofanya hivyo itakuwa tunafanya kazi bure hata hiyo miundombinu ambayo tunaijenga kwa gharama kubwa haita saidia maana maji yatakuwa hakuna bila kutunza vyanzo vyetu”, alisema Waziri Profesa Mbarawa.
“Hali ya upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Kilindi, Mkinga, Korongwe, Handeni hairidhishi hivyo basi serikali inafanya jitihada za makusudi ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata majisafi na Salama” alisema.
Akiwa Kilindi waziri alishuhudia kukuta mradi wa ujenzi wa tanki la maji umekamilika lakini pampu imeungua na wananchi hawapati maji. Waziri amemuagiza mkandarasi aliyejenga mradi huo kuhakikisha kuwa ifikapo Ijumaa tarehe 1 Machi, 2019 awe amefunga pampu hiyo na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.
Aidha, Waziri alisema katika maeneo mengi aliyopita ameona kuwa changamotoo kubwa ya miradi ya maji inasababishwa na wataalam wetu kwa sababu ya kuwapa fursa Wakandarasi ya kufanya chochote wanachotaka hivyo amewataka wataalam kuwa waadilifu na kusimamia miradi hiyo kwa ukaribu zaidi.
Ameeleza kuwa Wizara ipo katika mchakato wa kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini mfano wake kama TARURA ambaye anasimamia barabara za vijijini. Tunaamini TARURA anafanya vizuri na sisi tukienda kwenye mfumo huo wa kuwa na Wakala wa Maji Vijijini nasi tutafanya vizuri.
Akiwa katika mji wa Mombo Waziri Mbarawa alikutana na Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Mary Chatanda ambaye alimueleza kilio kikubwa cha wananchi wake kuwa ni maji.
Waziri alisema ameipokea changamoto hiyo na amemuahidi kuwa Wizara itatoa Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya kumpatia Mkandarasi Saxon Building ili aendelee na ujenzi wa miradi ya Rwegela na Msambiazi iliyopo Korogwe mjini.
Waziri wa Maji, Mhe. Makame Mbarawa alipata fursa pia ya kuzungumza na wananchi wa Tanga kupita redio ya Tanga Kunani moja kwa moja.
Wananchi wengi wa Tanga walitoa vilio vyao kuhusu kero ya maji hasa katika Halmashauri za Mkinga na Handeni na sehemu nyingine.
Waziri ameahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo na kusema kuwa hali halisi amejionea mwenyewe na Serikali itajitahidi kuondoa changamoto hizo ili wananchi wapate maji safi na salama.
No comments:
Post a Comment