Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe (hawapo pichani)
wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la
kuhimiza uwajibikaji kabla ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani
Kisarawe.
.........................
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
amewataka watumishi wa umma nchini kutotumika kisiasa kwani uwepo wao una lengo
mahususi la kuboresha utoaji huduma wenye viwango stahiki ikiwa ni pamoja na
kuijenga Serikali ili iweze kuleta maendeleo kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri huyo
wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe chenye
lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla ya kutembelea wanufaika
wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Kisarawe ili kujiridhisha na
utekelezaji wa mpango huo.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, serikali
inahitaji utaalam wa watumishi wa umma katika kujenga utumishi wa umma imara
uliotukuka, utumishi ambao utaziwezesha taasisi za umma zote nchini kutoa
huduma stahiki kwa wananchi.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza kuwa,
hategemei kumuona mtumishi wa umma yeyote akijihusisha na siasa zinazosababisha
kukwamisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwahudumia wananchi wake
kikamilifu.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka
Makatibu Tawala wa Mikoa kuwasimamia kikamilifu Wakurugenzi Watendaji wa
Halmashauri ili kujenga ushirikiano wa kiutendaji kati ya Makatibu Tawala wa
Wilaya na Wakuu wa Wilaya kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa umma.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amehimiza
ushirikiano wa watendaji hao ili kurahisisha utendaji kazi wa shughuli za
serikali kwa ujumla, na kuongeza kuwa, serikali iliyopo madarakani ni moja tu
inayoongozwa na Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli, hivyo anashangaa inakuwaje Makatibu
Tawala wa Wilaya wasiarifiwe masuala yanayoendelea katika halmashauri.
“Kuanzia sasa barua yoyote ya
kiutendaji itakayotoka mkoani kuelekezwa kwa Wakurugenzi Watendaji wa
Halmashauri, ni lazima nakala ya barua hiyo ielekezwe pia kwa Makatibu Tawala
wa Wilaya ili wafahamu kinachoendelea na kumuarifu Mkuu wa Wilaya kufanya
ufuatiliaji wa utendaji kazi’, amesisitiza Dkt. Mwanjelwa.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameyasisitiza
yote hayo wilayani Kisarawe ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi yenye
lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma Mkoani Pwani ambapo mpaka
hivi sasa ameshakutana na watumishi katika Halmashauri ya Mji Kibaha,
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri
ya Wilaya ya Chalinze na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na wananchi na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Jokate Mwegelo, wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa Halmashauri hiyo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akishuhudia
baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na wanufaika wa TASAF katika kijiji cha Kitanga
wilayani Kisarawe wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF wilayani humo. Aliyeambatana naye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe,
Mhe. Jokate Mwegelo.
No comments:
Post a Comment