Tuesday, February 5, 2019

BILIONI 1.5 KUTUMIKA KATIKA UJENZI WA HOSPITALI YA KISASA WILAYANI KIBAHA MKOANI PWANI

 Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka akizungumza jambo na waandishi wa habari hawapo pichani katika eneo ambalo limetengwa maalumu kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa hospitali ya Wilaya ambayo imeanza kujengwa katika eneo la Lulaniz kata ya picha ya ndege

 Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka akizungumza na wananchi wa kata ya picha ya ndege katika mkutano wa hadhara mara baada ya kufanya ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Wilaya ambayo inajengwa katika eneo la mtaa wa Lulanzi.
.................................................

VICTOR MASANGU, KIBAHA

KATIKA  kukabiliana na changamoto ya utoaji wa huduma ya afya kwa wananchi wa Wilayani Kibaha Mkoani Pwani serikali ya awamu ya tano imeamua kujenga hospitali mpya ya kisasa katika eneo la kata ya Picha ya ndege kwa lengo la  kuwaondolea kero ya siku nyingi ya kutembea umbari mrefu kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na ujenzi huo Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Lulanzi inapojengwa hospitali hiyo Thobiasi Shilole alisema  kuwa kukamilka kwa mradi huo utaweza kuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa maeneo mbali mbali ya Kibaha kwani hapo awali walikuwa wanapata usumbufu mkubwa pindi wanapohitaji huduma ya matibabu.


Kwa upande wake Mbunge wa Kibaha mjini Silvestry Koka ambaye amefanya ziara yake ya kikazi kwa ajili ya  kukagua na kujionea  mwenendo  mzima wa  eneo hilo la ujenzi na kumpongeza Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli kwa kuamua kutoa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ya ujenzi huo na kuwataka wakandarasi kuhakikisha wanajenga majengo yenye ubora unaotakiwa  na kuachana na tabia ya kufanya kazi  ambazo zipo chini ya kiwango.
 
Koka alibainisha kwamba kujengwa kwa mradi huo wa ujenzi wa hospitali ni kutokana na juhudi ambazo alizifanya kwa kushirikiana na viongozi mbali mbali  wa wilaya pamoja na serikali  kuu kwa ujumla na kuahidi kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi katika sekta mbali mbali.

“Huu mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya kwa kweli umeletwa kwetu kwa lengo la kuwasaidia wananchi katika suala zima la kuwasogezea huduma ya matibabu, kwa hivyo mimi kama Mbunge ninatoa pongezi zangu za dhati kabisa kwa Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli katika kuwaboreshea wananchi huduma ya afya pamoja na mambo mengine,”alisema Koka.

Naye Diwani wa kata ya Picha ya ndege Robert Machumbe akizungumza na wananchi mara baada ya kutembelea eneo hilo la mradi amebainisha kuwa nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuwaletea wananchi  mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika nyanja mbali mbali ambapo kwa sasa wameshapata  eneo lenye ukumbwa wa Hekari 25 kwa ajili ya ujenzi  wa hospitali hiyo ya Wilaya.

“Kwa kweli tunapenda kuishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuweza kutuletea mabadiliko chanya ya kimaendeleo ambapo utaona kwa sasa katika kata hii ya picha ya ndege kuna hatua kubwa sana ambayo tumeifanya katika nyanja mbali mbali na sasa tumeshaanza ujenzi wa hospitali yetu ya Wilaya ambayo itajengwa katika mtaa wa Lulanzi kwa hivyo hii ni hatua kubwa sana pamoja na shule ya sekondari ambayo tayari eneo la hekari 11.7 limeshapatikana,”alisema.

 KUKAMILIKA kwa ujenzi huo wa hospitali ya Wilaya kwa wananchi  wa Kibaha mkoani Pwani na maeneo mengine ya jirani  kutaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuondokana na changamoto ya kutembea umbari mrefu kwa ajili ya kwenda kutafuta huduma ya afya katika maeneo mengine.
 
 Mwenyekiti wa mtaa wa Lulanzi Thobisi Shilole akifafanua jambo kwa waandishi wa habari hawapo pichani mara baada ya kutembelea eneo la ujenzi ambalo limetengwa kwa ajili ya hospotali ya Wilaya katika eneo la mtaa wa Lulanzi.

 Diwani wa kata ya picha ya ndege Robert Machumbe akizungumza jambo katika mkutano na wananchi kuhusiana na ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na masuala mbali mbali yaliyafanyika katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tani (PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU.

No comments:

Post a Comment