NA MWAMVUA MWINYI, KIBITI
MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo ametoa muda
wa mwezi mmoja kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Kibiti na mkuu wa wilaya hiyo
kuhakikisha ujenzi wa hospital ya wilaya unaanza mara moja.
Amesema haiwezekani fedha kiasi cha sh. bilioni 1.5 zipo,
pamoja na eneo lakini cha kushangaza eneo limeachwa badala ya kuanza utekelezaji.
Akitoa maelekezo hayo wakati alipokwenda kutembelea eneo la
ujenzi huo huko Mtawanya, Ndikilo alisisitiza wajipange na kuanza ujenzi mara
moja.
Alisema, baada ya mwezi mmoja atakwenda kuangalia kama
maagizo aliyotoa yamefanyiwa kazi.
“Eneo mnalo haiwezekani liwe jeupe namna hii, pesa ipo
nataka watu waingie kazini, “
“Halmashauri ya Kibaha Mjini na Vijijini wameshaanza ujenzi
na wanaendelea vizuri, mkurugenzi hapa, Dc kimya, najua ni wachapa kazi,
fanyeni vitendo kama tulivyozoea kuwaona “alisisitiza Ndikilo.
Hata hivyo ,Ndikilo alifafanua mkoa umepokea bilioni 4.5 kwa
ajili ya hospital hizo tatu.
Alielezea kwamba mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji
umeme stigler’s gorge (Stigo) atatumia barabara ya Kibiti -Mloka hivyo
idadi kubwa itatumia hospital hiyo, ambapo itakuwa mkombozi kwa wananchi walio
wengi.
Pia aliipongeza halmashauri ya wilaya ya Kibiti ,kwa kuanza
ujenzi wa ofisi ili kumuondolea kero mkurugenzi ya kupangisha kwenye
ofisi za watu binafsi kwa ajili ya watumishi wa halmashauri ambao hurundikana
kwenye ofisi hizo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kibiti, Alvera
Ndabagoye alisema wamejipanga kuanza ujenzi wa hospital ya wilaya.
Mkuu wa wilaya ya Kibiti, Gulam Kifu alibainisha wamepokea
maelekezo waliyopatiwa na mkuu wa mkoa huyo na ameahidi kuyafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment