Wakulima wa mpunga wapatao 28
wanachama wa skimu ya Umwagiliaji BIDP maarufu kama Skimu ya Jitegemee iliyopo
Kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyo, wamemlalamikia Mkandarasi anayetekeleza
mradi wa ujenzi wa barabara na mifereji ya maji katika skimu hiyo kwa kuwatia
hasara kwa kusua sua kwa utekelezaji wa mradi huo.
Mkandarasi huyo toka kampuni ya
musons engineers alianza kutekeleza mradi huo Mwezi April 2018 na alitarajiwa
kukamilisha mradi mwishoni mwa Mwezi Novemba, 2018 lakini hadi sasa
hajakamilisha mradi huo na anaendelea kuutekeleza akiwa katika kipindi cha
adhabu ambacho pia kinakwisha ifikapo tarehe 18 Februari, 2019.
Wakulima hao 28, waliwasilisha
malalamiko yao kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Waheshimiwa madiwani ya Uchumi,
Ujenzi na Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Hapsa Kilingo
ambaye aliongoza wajumbe wa kamati hiyo waliofuatana na Wataalam wa Halmashauri
kuutembelea na kuukagua mradi huo wa ujenzi wa mifereji na barabara katika
Skimu ya Umwagiliaji ya Tegemeo mapema jana.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima
wenzake wa skimu ya Tegemeo, mmoja wa wakulima (jina limehifadhiwa) anayefanya
shughuli zake za kilimo katika Skimu hiyo kwenye kitalu GH amesema, yeye na
wakulima wenzake wa kitalu GH ndio wahanga wakubwa zaidi, kwani tangu msimu wa
pili wa kilimo uanze hawajafanikiwa kabisa kupata maji katika mashamba yao,
kutokana na mkandarasi kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati, hususani ujenzi
wa mifereji ya kupeleka maji katika kitalu hicho, hali iliyopelekea wakulima 28
wa kitalu GH kupata hasara kubwa ya kuunguliwa na mazao yao.
“Wakati wenzetu wakikaribia kuvuna
mpunga katika mashamba yao, sisi hatuna kabisa matarajio hayo ya kupata chakula
katika msimu huu, ni maumivu makubwa sana kwa mkulima kulima kisha akakosa
mavuno kwa sababu za uzembe tu wa mkandarasi aliyeamua kufanya kazi bila
kuzingatia mahitaji halisi ya wakulima lakini pia kwa kusua sua sana hivyo
kupelekea mradi kutokamilika kwa wakati, niwaombe viongozi watusaidie kuhakikisha
mradi huu unakamilika ili tuondokane na changamoto hizi” Anaongeza Mkulima
huyo.
Nae diwani wa Kata ya Magomeni
unakotekelezwa mradi huo Mhe. Mwanaharusi Jarufu akizungumza
katika Ziara hiyo ameonesha kutoridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa mradi
wa ujenzi wa mifereji na barabara katika Skimu hiyo, na kueleza kwamba mradi
umetekelezwa chini ya kiwango na ni vyema Mamlaka zinazohusika kufika katika
mradi huo na kuukagua kuona kama mradi umetekelezwa katika kiwango
kinachotakiwa, kwani hayuko tayari kuona fedha za Serikali zinapelekwa katika
Kata anayoiongoza na kisha fedha hizo zisifanye kile kilichotarajiwa na
Serikali.
Akizungumza na Wakulima hao mara
baada ya kukagua mradi huo na kusikiliza kero za wakulima wa skimu hiyo,
Mwenyekiti wa kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Mhe. Kilingo amewaasa
wakulima hao kuwa watulivu na wavumilivu wakati kamati yake na Ofisi ya
Mkurugenzi ikiendelea kushughulikia suala lao kwa haraka kwa kufanya mazungumzo
na mkandarasi ili akamilishe mradi huo mapema iwezekanavyo.
Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira
jana imefanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ya Sekta za Kilimo na
Ufugaji ikiwa ni katika utaratibu wake wa kawaida wa kutembelea na kukagua
miradi ya maendeleo kila robo.
Wakulima wa mpunga wapatao 28 wanachama wa skimu ya Umwagiliaji BIDP maarufu kama Skimu ya Jitegemee iliyopo Kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyo wakilalamikia mbele ya Madiwanai, kukosa maji kwenye mashamba yao baada ya mkandarasi anaetengeneza barabara na mifereji ya maji kuchelewa kukamilisha kazi yake.
Mmoja
wa wakulima hao akiwaonyesha Madiwani namna mifereji ilivyoharibika na
kupelekea kukosa maji ya kumwagilia mashamba yao, hiyo ni baada ya mkandarasi
aliyepewa kazi kuchelewa kukamilisha kazi yake, mwenye mtandio mweupe ni Diwani wa kata ya Magomeni Mwanaharusi Jarufu.
kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, ya Halamashauri ya Bagamoyo wakitembelea mashamba ya mpunga ambayo yamekosa maji kutokana na Mkandarasi kuharibu mifereji ya maji na kuchelewa kukamilisha kazi yake ya ukarabati.
Muonekano
wa mifereji ya maji ya kumwagilia kwenye mashamba ya mpunga kama inavyoonekana
ikiwa imeharibika mara tu baada ya kutengezwa ambapo kampuni inayofanya kazi
hiyo baado inaendelea na kazi huku wakulima wakilalamika kukosa maji ya
kumwagilia kwenye mashamba yao.
Diwani
wa Viti Maalum Tarafa ya Mwambao Shumina Rashidi, akiandika baadhi ya hoja zilizotolewa na wakulima
wa mpunga katika shamba hilo wakati kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, ya Halamashauri ya Bagamoyo.
Mwenyekiti wa kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Hapsa Kilingo (katikati) akimsikiliza mmoja wa wakulima akiwaonyesha mifereji ya maji ilivyoharibika hali inayopelekea wakulima kukosa maji kwenye mashamba yao, kushoto ni Diwani
wa Viti Maalum Tarafa ya Mwambao Shumina Rashidi.
Muonekano
wa shamba ambalo limekosa maji na mpunga kunyongea na Ardhi yake kupasuka kama inavyoonekana.
No comments:
Post a Comment