Februari 25, 2019
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linawaomba radhi Wateja wake wa Mkoa
wa Dar es salaam kwa kukosa huduma ya umeme kwa siku za hivi karibuni
kutokana na maboresho makubwa yanayohusisha matengenezo kinga ya mashine
3 za Kituo cha Ubungo II, pamoja na uwekaji wa transfoma kubwa la MVA
300 kwenye Kituo cha kupoza umeme cha Ubungo ili kukiongezea uwezo na
kwenda sambamba na ukuaji wa mahitaji ya jiji la Dar es Salaam.
Kabla ya matengenezo kuanza mnamo Januari 2019 Kituo hiki cha kupoza
umeme cha Ubungo kimekuwa kinapokea umeme kutoka katika vituo vya
Uzalishaji umeme vilivyopo upande wa msongo wa kilovolti 220 kupitia
transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 150 kila moja, zenye kupokea umeme wa
msongo wa Kilovolti 220 na kuushusha hadi kuwa msongo wa Kilovolti
132 katika transforma namba sita na namba saba za kituo cha Ubungo na
vituo vya uzalishaji umeme vilivyoungwa kwenye msongo wa kilovolti 132
ambavyo vimeungwa moja kwa moja kwenye mfumo mkuu wa usambazaji umeme
kwa Dar es Salaam na Zanzibar.
Kutokana na matengenezo yanayoendelea vituo vya uzalishaji umeme
vilivyoungwa kwenye msongo wa kilovoti 132 na 33 vimekuwa nguzo kubwa ya
upatikanaji wa umeme. Vituo hivyo ni Ubungo II na Tegeta.
Shirika kupitia wataalamu wake tayari limefanya jitihada kubwa za
kupunguza athari za upungufu wa upatikanaji wa umeme kwa wakaazi wa Dar
es salaam na Zanzibar kwa kufanya yafuatayo:
Mosi, Kufungua laini ya msongo wa kilovoti 132 kati ya Kilimanjaro na
Hale: Hili hufanyika ili kutoruhusu umeme wa kutoka Dar es Salaam na
Morogoro kwenda Kilimanjaro hivyo Mkoa huu kuchukulia kwenye upande wa
msongo wa kilovolti 220 kutoka Arusha.
Pili , Kuwezesha upatikanaji wa umeme katika baadhi ya maeneo ya Mkoa
wa Dar es salaam, kwa kuunga baadhi ya njia za Usafirishaji umeme
kutoka Kituo cha Kinyerezi, Gongolamboto hadi Mbagala ili kuwezesha
maeneo hayo kupata umeme bila kupitia kituo cha Ubungo ambacho kipo
katika matengenezo.
Tatu, Kufungua njia ya umeme ya kilovolti 132 itokayo Kituo cha
Kunduchi hadi Mlandizi na kuunga maeneo hayo katika njia ya umeme ya
kilovolti 132 itokayo Morogoro ili kuwezesha jiji la Dar es salaam kuwa
na umeme wa uhakika.
Nne, Kufungua laini ya msongo wa kilovolti 132 kati ya Ubungo na
Chalinze upande wa Ubungo ili kutozihusisha transfoma za Ubungo kwenye
mzigo wa mikoa mingine na hivyo kutumika kuhudumia wateja wa Dar es
Salaam na Zanzibar pekee.
Tunatarajia matengenezo haya yanayokwenda kwa awamu yatakamilika ifikapo mwezi Juni 2019.
TANESCO itaendelea kutoa taarifa ya Maendeleo ya kazi ya matengenezo ya
kituo cha Ubungo yenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa umeme wa
uhakika Dar es salaam na Zanzibar kwa siku zijazo
Kituo cha miito ya simu 2194400 na 0768 985100
Tovuti: www.tanesco.co.tz,
Mitandao ya kijamii
Twitter, www.twitter.com/tanescoyetu,
Facebook https://www.facebook.com/tanescoyetultd/
IMETOLEWA NA:
OFISI YA UHUSIANO
TANESCO MAKAO MAKUU
No comments:
Post a Comment