Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Zainab Chaula akisema jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa
wataalam wa udhibiti ubora wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA na Wakala
wa Chakula, Dawa na vipodozi Zanzibar (ZDFA) Jijini Dar Es Salaam.
Picha ya Pamoja wajumbe wakiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula
(aliyeketi wa tatu kulia)
Na WAMJW- Dar es Salaam
TANZANIA
yatajwa miongoni mwa nchi 50 kati ya 194 duniani zenye mifumo imara na
madhubuti ya udhibiti wa ubora wa bidhaa za vyakula, dawa na vipodozi.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula leo wakati alipokuwa
akifungua mafunzo ya siku tano kwa wataalam wa udhibiti ubora wa Mamlaka
ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Wakala wa Chakula, Dawa na
Vipodozi (ZDFA) na wenzao kutoka nchi ya Malawi.
Mafunzo hayo
maalum yameandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO-Tanzania) kwa lengo
la kuwaongezea mbinu mbalimbali zitakazowasaidia kuimarisha nchi hizo
kuongeza nguvu ya udhibiti wa bidhaa hizo.
“WHO imetutambua na
imetupa level (daraja) la tatu, hii ni hatua nzuri, TFDA imefanya kazi
kubwa, hii inamaanisha mifumo ya udhibiti tanzania inatambulika duniani
kote na kwamba misingi ya udhibiti ya mamlaka yetu imefikia ngazi ya
kimataifa". Amesema Dkt. Chaula na kuongeza “Lakini pamoja na hatua hiyo
lazima iendelee kujiimarisha ili ikiwezekana tupande daraja tufikie
level 4 ambayo ndiyo kiwango cha juu zaidi".
“Ili tuweze
kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi, mamlaka yetu inapaswa kutengeneza
mifumo ya ufuatiliaji ubora na usalama wa bidhaa kuanzia viwandani hadi
kwa mtumiaji, ili kuhakikisha hakuna dawa bandia zinaingia nchini
mwetu”.
Akiwasilisha mada Dkt. Alireza Khadem Broojerdi kutoka
WHO amesema ili kuongeza nguvu ya udhibiti nchi zinapaswa kushirikiana
kwa ukaribu.
“Tunayo malengo 17 ya kidunia (SDGs), lengo namba
tatu linasisitiza juu ya afya bora kwa wote, tunayo pia malengo ya mwaka
2019- 2030, mpaka sasa nchi 50 ikiwamo Tanzania sawa na asilimia 26
zimefikia daraja la tatu na nne. Nchi 45 sawa na asilimia 23 zipo daraja
la pili, nchi 96 zimefikia daraja la kwanza na zingine zilizobaki bado
hazijafikia viwango hivyo,” amesema Dkt. Khademu.
Awali
akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Dkt. Candida Shirima amesema
kupitia semina hiyo iliyoandaliwa na WHO watajifunza mbinu mbalimbali
zitakazowasaidia kuweza kufikia malengo waliyojiwekea katika kuendelea
kuimarisha mifumo ya udhibiti wa bidhaa hizo.
No comments:
Post a Comment