Na Beatrice
Lyimo-MAELEZO
DODOMA
Serikali imeamua kuanzisha minada ya kahawa
kwenye maeneo ya uzalishaji kuanzia msimu wa 2019/2020 ili kuinua zao hilo la
kimkakati nchini.
Hayo yamesemwa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri
wa Kilimo, Omary Mgumba wakati akijibu swali Mhe. Bernadeta
Mushashu kuhusu mpango wa Serikali wa kuinua zao la kahawa Mkoani Kagera
ikiwemo kupandisha bei ili kumnufaisha mkulima.
Mgumba amesema kuwa lengo la utaratibu huo ni
kuharakisha malipo na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa minada na
kuwashirikisha wakulima wengi zaidi katika mikoa inayozalisha kahawa ikiwemo
Mkoa wa Kagera.
Aidha, amesema kuwa katika kuboresha mazingira ya
biashara ya zao hilo, Serikali inadhibiti makato yasiyo ya tija kwa wakulima
yanayokatwa kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi ili kubaki na
makato yanayolenga kuendeleza zao la kahawa.
“Kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB),
Serikali imewezesha vyama vya ushirika vya kahawa kupata mikopo yenye riba
nafuu kwa ajili ya kufanikisha shughuli za ukusanyaji na uuzaji wa kahawa ya
wakulima hivyo kumpunguzia mkulima mzigo wa riba uliokuwa unatozwa na mabenki
ya kibiashara,” amefafanua Naibu Waziri Mgumba.
Hata hivyo, Mgumba ameongeza kuwa, Serikali imefuta tozo na
kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinatozwa kwa wakulima
ikiwa ni pamoja na kupunguza tozo zilizokuwa zinatozwa katika biashara ya
kahawa pamoja na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa
vinakusanywa na mkulima.
“Serikali pia imepunguza kiwango cha ushuru wa mazao unaotozwa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka asilimia tanohadi asilimia tatuya bei ya
kahawa shambani,” amesema Mgumba
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Innocent Bashungwa
akijibu swali la Mbunge wa Ziwani, Mhe. Nassoro Omar kuhusu mpango wa Serikali
kuhamasisha kilimo cha viungo vya chakula nchini amesema kuwa, Serikali
inatambua umuhimu wa mazao hayo kutokana na mchango wake katika kipato cha
mkulima mmoja mmoja na pia katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
“Kutokana na umuhimu huo, Serikali kwa
kushirikiana na Sekta binafsi imeandaa mkakati wa kuendeleza mazao ya viungo
(Spice Sub-Sector Strategy-2014) ambao unalenga kuongeza uzalishaji na tija
ukiwa na maeneo mahususi ya utoaji mafunzo ya kuongeza ujuzi katika uzalishaji
kwa wataalamu wa wakulima, uanzishaji wa vituo vya kukusanyia mazao na kupanga
madaraja na kuunda masoko ya pamoja ya wakulima,” amefafanua Naibu Waziri
Bashungwa.
Ameongeza kuwa, Serikali imeandaa Mwongozo wa
uzalishaji wa mazao ambao umeainisha maeneo yanayofaa kwa uzalishaji wa mazao
mbalimbali yakiwemo ya viungo ambao umalenga kuonesha fursa za uzalishaji wa
mazao hayo.
Zao la kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati
yanayoliingizia Taifa fedha zakigeni sambamba na korosho, pamba na chai.
No comments:
Post a Comment