Wednesday, February 6, 2019

WAUGUZI WANNE KITUO CHA AFYA WASIMAMISHWA KAZI KUTOKANA NA KUTOA LUGHA CHAFU KWA MGONJWA.

NA MWAMVUA MWINYI, BAGAMOYO

SERIKALI mkoani Pwani pamoja na idara ya afya mkoani humo,imewasimamisha kazi wauguzi wanne katika kituo cha afya kiitwacho Mkoani ,baada ya kudaiwa kutoa lugha chafu kwa mama aliyempeleka mtoto wake aliyekuwa amekwamwa na chaki kooni.

Aidha mkoa huo imeelekeza fedha kiasi cha sh. milioni 400-500 zinazopelekwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya zitumike vizuri bila ubabaishaji.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo aliyasema hayo, wakati alipotembelea kituo cha afya cha Matimbwa kata ya Yombo, Bagamoyo kuangalia ujenzi unavyoendelea,na kusema wauguzi hao ni wale waliokuwa zamu siku ya tukio .

Alisema, wauguzi hao wamewasimamisha wiki iliyopita na tayari wameandika barua za kujieleza ,ambapo vimeundwa vyombo vya uchunguzi kujua chanzo na ukweli wa jambo hilo.

Ndikilo alisema, endapo wakibainika kuhusika na kitendo hicho hatua itachukuliwa ili iwe fundisho kwa wengine .

“Baada ya kufikishiwa malalamiko hayo kutoka kwa mama wa mtoto, nilikutana na mganga mkuu wa mkoa, katibu afya, mkurugenzi wa halmashauri na muuguzi mkuu kujadili suala hilo na kuchukua hatua za awali “

“Wahusika wameandika barua za kujieleza, na kati ya hao wengine tumegundua mafaili yao yanaonyesha kupewa onyo mara kadhaa kutokana na tabia hiyo hiyo. “alifafanua Ndikilo.

Mkuu huyo wa mkoa, alieleza serikali inaelekeza nguvu zake kuboresha huduma za afya kwa kutoa mabilioni ya fedha, hivyo vituo vya afya vyote viendane na utoaji wa huduma bora.

Nae mganga mkuu wa mkoa wa Pwani, dokta Gunini Kamba alisema inadaiwa mama huyo alipoona karushiwa maneno makali na wauguzi hao aliondoka kwenda hospital nyingine na baadae aliamua kwenda kutoa malalamiko hayo ambayo yameanza kuchukuliwa hatua hizo.

Alitoa onyo kwa watumishi na wauguzi wa afya ambao wanakiuka taratibu na maadili waliyopatiwa.

No comments:

Post a Comment