Tuesday, February 5, 2019

BAGAMOYO NI MIONGONI MWA HALMASHAURI 12 ZITAKAZOFAIDIKA NA BILIONI 137 ZA SERIKALI KATIKA KUTEKELEZA MIRADI YA KIMKAKATI

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia), akikabidhi Hati ya makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa kimkakati katika Mkoa wa Pwani, wa pili kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bi. Theresia Mmbando, wakati wa hafla ya utiaji saini wa miradi hiyo iliyofanika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, akieleza kuhusu Halmashauri zilizokidhi vigezo vya kupewa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati yenye thamani ya Sh. bilioni 137.38, kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo kwa lengo lililokusudiwa, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
............................


Na  Saidina Msangi, WFM, Dodoma

Serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imezipatia Halmashauri 12 nchini ruzuku ya shilingi bilioni 137 kwa ajili ya kutekeleza Miradi 15 ya kimkakati, yenye lengo kuhakikisha Halmashauri zinaongeza mapato ya ndani  na kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka Serikali Kuu.

Hafla ya uwekaji wa saini mikataba ya ruzuku hiyo imefanyika Jijini Dodoma kati ya Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Doto James na wakurugenzi wa Halmashauri huku ikishuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Dkt. Doroth Gwajima na baadhi ya Makatibu Tawala wa Mikoa ambao Halmashauri zao zimepata ruzuku hiyo.

Katibu Mkuu Bw. Doto James amezitaka Halmashauri  zilizopata fedha hizo kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa na kuonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watendaji watakao kiuka makubaliano yaliyomo kwenye Mkataba wa makubaliano.

“Maafisa Masuuli mhakikishe mnafuata na kuzingatia Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015 na Kanuni zake, ambayo pamoja na mambo mengine inasisitiza juu ya matumizi bora ya fedha kwa shughuli zilizoidhinishwa” alisisitiza Bw. James. 

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, ilipoanzisha utaratibu huu haikuwa inatania wala kufanya mazingaombwe, inayo dhamira ya dhati ya kuzijengea uwezo halmashauri zijitegemee kiuchumi na kutoa huduma bora kwa wananchi badala ya kutegemea ruzuku ya Serikali Kuu na kuwahakikishia wadau kuwa fedha hizo zipo na kuzitaka Halmashauri zichangamkie fursa hiyo kikamilifu

Miradi inayotarajiwa kutekelezwa  inahusisha masoko ya kisasa, kiwanda cha kusindika korosho, uendelezaji wa fukwe ya Oysterbay pamoja na maegesho ya malori, iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Kigamboni, Tanga, Kibaha, Bagamoyo, Mwanza, Tarime, Hanang, Iringa na Biharamulo.

Kwa upande wake Kamishina wa Bajeti wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga amesema Awamu ya Pili ya Miradi ya Kimkakati kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa miradi iliyokidhi vigezo ni  15 yenye thamani ya Sh. Bilioni 137.38.

Amesema kuwa katika Awamu ya Kwanza ya Mpango huo wa Serikali wa kuzijengea uwezo Halmashauri kutekeleza miradi ya kimkakati kwa Mwaka wa Fedha 2018/2018, Halmashauri 17 zenye miradi 22 zilifuzu vigezo na kupatiwa ruzuku ya shilingi bilioni 131 hivyo kufanya miradi yote mpaka sasa kufikia 37 ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 268.38

Naye Naibu Katibu Mkuu, kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI, Dkt. Doroth Gwajima, ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha ambazo zitachochea miradi ya maendeleo katika Halmashauri nchini.

Dkt. Gwajima, amezitaka Halmashauri zilizofanikiwa kusaini mikataba hiyo, kuhakikisha kuwa zinazingatia lengo la mkataba huo na kutekeleza miradi kwa muda mwafaka na viwango vilivyoainishwaa na kwamba ufuatiliaji wa miradi hiyo utakuwa ni wa kiwango cha juu.

Pia amekiagiza Chuo cha Serikali za Mitaa – Hombolo, kuandaa mafunzo ya kuzijengea uwezo Halmashauri nchini ambazo hazikufanikiwa katika uandikaji wa miradi ili ziweze kufanikiwa kwa awamu ijayo.
 
 Makatibu Tawala wa Mikoa  kutoka kushoto ni Bi. Zena Said  wa Tanga, Theresia Mmbando, Pwani na Bi Happiness Seneda wa Iringa wakizungumza jambo katika hafla ya uwekeji saini wa miradi ya kimkakati ya Awamu ya Pili kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa iliyofanika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, akisaini mikataba ya miradi 15 ya Kimkakati ya awamu ya pili kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa,  hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.

 Wakuu wa Idara na Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango, wakishuhudia uwekaji saini wa miradi ya kimkakati ya awamu ya pili kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
 Uwekaji saini wa mikataba ya miradi 15 ya Kimkakati ya Awamu ya Pili kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ukiwemo mkoa wa Iringa uliofanyika, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.

 Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dkt. Doroth Gwajima, akitoa maelekezo mbalimbali kwa Halmashauri zilizopata ruzuku kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, kuhusu namna bora ya kutekeleza miradi hiyo kwa viwango na ubora wa hali ya juu, Jijini Dodoma.
 
 Wadau mbalimbali wa miradi ya Kimkakati ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa wakiwa katika hafla ya uwekeji saini wa Mikataba ya miradi hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.


 Mhasibu Mkuu wa  Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 21, Bw. Sayi Nsungi (kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa Mifumo ya Kifedha Bw. Hamza Rashid, wakifurahia jambo wakati wa hafla ya uwekeji saini mikataba ya miradi ya kimkakati ya Awamu ya Pili kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa iliyofanika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment