|
Anna Sangai akzungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya Ukatili
dhidi ya watoto |
|
Sehemu ya wageni waliohudhuria mkutano wa kampeni ya ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili wa Kingono
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
25 February 2019
KAMPENI YA ULINZI WA MTOTO DHIDI YA
UKATILI WA KINGONO- “1-5-5 NAMLINDA”
“Mlinde
mtoto afurahie utoto wake, ujana wake na uzee wake”
Ukatili
dhidi ya watoto umekuwa ni sehemu ya maisha ya watoto wengi nchini. Mojawapo ya aina za
ukatili unaokumba kundi hili ni ukatili
wa kingono.
Mnamo mwaka 2011, nchi yetu
ilitoa taarifa ya utafiti uliofanyika kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto,
utafiti huo uligundua kuwa karibia mmoja kati ya wasichana watatu na mmoja kati
ya wavulana saba wamekutana na ukatili wa kingono kabla ya kutimiza miaka 18.
Hata hivyo, kulingana na utafiti huo, wengi wa watoto hawatoi taarifa juu ya vitendo hivyo,
wachache wanatafuta huduma na wachache
zaidi wanafanikiwa kupata matibabu au msaada wanapotoa taarifa ya matukio hayo.
Pia, ripoti iliyotolewa na Kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) zinaonyesha
kuwa matukio ya ukatili wa kingono miongoni mwa watoto yanaongezeka nchini.
Kulingana na ripoti hiyo
iliyotolewa Juni 2018, wastani wa watoto 394 wamebakwa kila mwezi katika maeneo
mbalimbali Tanzania bara, huku ulawiti wa watoto ukiongezeka kutoka matukio 12 kwa kipindi cha Januari hadi Juni
2017 hadi matukio 533 kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2018, na mikoa inayoongoza
kwa matukio hayo ni Dar es salaam na Iringa.
Vitendo
hivi havikubaliki katika jamii kwani ni kinyume cha haki za binadamu na mikataba
mbalimbali ya kimataifa, na kikanda iliyoridhiwa na serikali juu ya ulinzi wa mtoto
dhidi ya aina zote za ukatili wa kijinsia. Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba
wa haki za mtoto wa mwaka 1989, tamko la Afrika juu ya haki na ustawi wa mtoto la
mwaka 1990.
Vitendo
hivi vinarudisha nyuma maendeleo ya mtoto na taifa kwa ujumla. Miongoni mwa
athari zitokanazo na ukatili wa kingono dhidi ya watoto ni pamoja na watoto
kuathirika kisaikolojia, maambukizi ya magonjwa ya zinaa na UKIMWI, mimba za utotoni,
na kubwa zaidi ni kuhatarisha ustawi wa taifa na kuchochea uongezeko la vitendo
hivi katika jamii.
Kutokana
na takwimu hizo, hali ya tatizo ni kubwa sana, jambo ambalo limesukuma TGNP
Mtandao kuja na kampeni ya ulinzi wa mtoto iitwayo 1-5-5 Namlinda. Kampeni hii inachangia katika jitihada za serikali
kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza
dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) unaolenga kupunguza ukatili dhidi ya
wanawake na watoti kwa asilimia 50 ifikapo 2022.
Kampeni
hii inalenga kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za ukatili wa
kingono kwa watoto na umuhimu wa kuwalinda dhidi aina hiyo ya ukatili,
kutathmini na kuibua mijadala katika jamii juu ya hali halisi ya ukatili wa
kingono, kuhamasisha jamii kuzuia vitendo hivi visitokee na kutoa taarifa
mara waonapo matukio hayo ya ukatili wa
kingono kwa watoto ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Kampeni
hii pia inalenga kujenga nguvu za pamoja na wadau mbalimbali nchini katika
kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili wa kingono na kuhakikisha
kila mtu katika jamii anajisikia kuwajibika kumlinda mtoto. Hivyo, kampeni hii
imelenga kuwafikia wanawake, wasichana, wavulana, wanaume, viongozi wa dini,
serikali, jamii, vyombo vya habari, madawati ya jinsia polisi, asasi za kiraia,
wadau wa maendeleo, makungwi, watoa huduma za afya,wanaharakati, watoa huduma
za usafiri wa umma kama bodabodaa na daladala pamoja na wabunge, na wanasiasa.
Kampeni
hii inatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 27 Februari 2019 ambapo wawakilishi wa
wadau mbalimbali ambao ni walengwa wa kampeni watashiriki ili kupitishwa katika kampeni hii na kujadiliana
kwa pamoja wajibu wa kila kundi katika ulinzi wa mtoto. Kampeni hii inatarajiwa
kuzinduliwa rasmi na mkuu wa jeshi la
polisi Tanzania-IGP Saimoni Sirro.
Jamii
inawajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.
Hii ni kwa mujibu wa sheria ya mtoto na. 21 ya mwaka 2009 na mpango kazi wa
taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
TGNP
Mtandao, inaamini kuwa ikiwa kila mtu
katika jamii atatimiza wajibu wake vizuri wa kumlinda mtoto, Tanzania billa
ukatili wa kingono kwa watoto inawezekana. Pia, TGNP inaamini kuwa ikiwa watoto
watakuwa huru dhidi ya aina zote za ukatili wa kijinsia, tutakuwa na taifa
imara lenye viongozi bora, nguvukazi iliyo na afya njema na tutaweza kufikia malengo
ya dunia ya maendeleo endelevu. Madai yetu katika kampeni hii ni pamoja na:-
Kuitaka jamii kuguswa na tatizo la ukatili
wa kigono kwa watoto wakiwa nje na ndani ya shule
Jamii ichukue hatua za kumlinda mtoto
popote alipo. Kila mmoja alipo asimamie ulinzi wa mtoto
vyombo vya habari vitoe elimu kwa wingi
juu ya athari za ukatili wa kingono kwa watoto, faida ya kuwalinda watoto na
kuendelea kukemea vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya watoto.
Serikali kuu, serikali za mitaa na vyombo
vya dola visimamie kikamilifu sheria ya kudhibiti uchawi na. 12 ya mwaka 1998(The Witchcraft Act). Ambayo imeainisha
adhabu kwa watu wanaoendesha vitendo vya kishirikiana vinavyoweza kuwadhuru
watoto na kuongeza vitendo vya ukatili wa kingono kama ubakaji.
Tunatoa rai kwa jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola kama wadau wa
kutekeleza MTAKUWAA (NPA) kuhakikisha watoto wanakuwa salama kwa kuimarisha
ulinzi katika maeneo yote yanayotajwa kuwa sio salama kwa watoto nchini.
Kupitia kampeni hii jamii yote, kupitia
mtu mmoja mmoja na kikundi inapaswa kumlinda na kuhakikisha ustawi wa mtoto.
Tunaitaka serikali na wadau kuzijengea uwezo
kamati za ulinzi wa watoto ili waweze kutimiza majukumu yao ikiwemo kubaini
maeneo hatarishi katika kijiji/ mtaa na kupanga mikakati ya kupunguza ukatili
dhidi ya wanawake na watoto.
Imetolewa
na
Lilian Liundi
Mkurugenzi Mtendaji
TGNP Mtandao.
Kwa
mawasiliano:Wasiliana nasi kupitia idara ya
mawasiliano na habari
1.
Monica John
Simu:
0652 267 611 Email: monica.john@tgnp.org
2.
Jackson Malangalila
Simu:
0657 479 490 Email: Jackson. malangalila@tgnp.org
No comments:
Post a Comment