Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Hadi kufikia Januari 30 mwaka huu
Serikali imenunua tani 214,269.7 za korosho ghafi zenye thamani ya shilingi
707,089,957,200.00 sawa na asilimia 89.3 ya lengo la uzalishaji wa msimu
wa korosho wa mwaka 2018/2019.
Hayo yameelezwa leo Bungeni, Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omari Mgumba alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Kawe, Mhe. Halima Mdee kuhusu tani ngapi zimenunuliwa na Serikali
mpaka sasa na wakulima wangapi na vyama vingapi vya msingi vimelipwa na vingapi
bado havijalipwa.
“Ununuzi wa korosho unafanywa na Bodi
ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambapo malipo yaliyolipwa na kuingizwa kwenye
akaunti za wakulima hadi tarehe 30 Januari, 2019 ni kiasi cha shilingi
424,849,405,110 zilizotokana na korosho za wakulima kiasi cha tani 134,535.9,”
alisema Mhe. Mgumba.
Ameendelea kusema, jumla ya wakulima
390,466 wamelipwa hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2019. Aidha vyama vya msingi
603 vimelipwa kati ya vyama vya msingi 605 vilivyohakikiwa.
Aidha amesema, zoezi la operesheni
korosho linaenda vizuri na linatarajia kukamilika ifikapo tarehe 15 Februari
mwaka huu.
Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko
ni taasisi ya kibiashara yenye lengo la kupata faida na mtaji wake unatokana na
ruzuku kutoka Serikalini na mikopo kutoka taasisi za Fedha kama Benki ya
Maendeleo ya Kilimo – TADB, NMB na CRDB.
Mnamo Novemba, 2018 Serikali
iliungana na msimamo wa wakuliwa wa kukataa bei zilizotolewa na kampuni za
ununuzi wa korosho, ambapo zilitangaza kununua korosho kwa bei ya kati ya
shilingi 2,717 na shilingi 1,900 kwa kilo ikiwa imeshuka kutoka zaidi ya
shilingi 3,600 ya msimu uliopita.
Aidha, Mhe. Rais Dkt. Magufuli
alitangaza Serikali kununua korosho hizo kwa shilingi 3,300 badala ya shilingi
3,000.
No comments:
Post a Comment