RAIS
wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akitoa salamu za
Mwaka Mpya wa 2019, Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu)
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuidumisha hali ya amani
na utulivu ambayo ndio msingi wa mafanikio yanayoendelea kupatikana hivi sasa
na yatakayopatikana hapo baadae.
Dk.
Shein aliyasema hayo leo katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2019
aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Zanzibar.
Rais
Dk. Shein alisema kuwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya mwaka 2018
mafanikio makubwa yamepatikana ambayo yamechangiwa na kuwepo kwa amani,
mshikamano, umoja na mapenzi yaliopo.
Katika
risala yake hiyo Rais Dk. Shein alieleza kuwa hali ya amani, umoja na
mshikamano uliopo nchini ni jambo muhimu linalowavutia Washirika wa maendeleo
ambao wanaridhika na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndio maana
wanaiunga mkono katika mipango yake ya maendeleo.
Alisema
kuwa hapana shaka kwamba iwapo amani, usalama na utulivu vitadumishwa na
kufanya kazi kwa bidii Washirika wa Maendeleo watakuwa pamoja na Zanzibar katika kuisaidia
ili kuweza kutekeleza malengo yaliyopangwa.
Rais
Dk. Shein alitoa shukurani kwa wananchi wote kwa kuunga mkono juhudiza serikali
za kuiletea maendeleo Zanzibar na kueleza kuwa
moyo wao huo wa umoja na mshikamano umewezesha kuimarisha vizuri hali ya uchumi
wa Zanzibar.
Hata
hivyo, Dk. Shein alitoa shukurani nyingi kwa wananchi wote kwa kuunga mkono
juhudi za Serikali za kuiletea maendeleo Zanzibar
ambapo moyo wao huo wa umoja na mshikamano umewezesha kuimarisha vizuri hali ya
uchumi wa Zanzibar.
“Tukiwa
tunaukaribisha mwaka mpya wa 2019, nachukua fursa hii kwa niaba ya wananchi
wote wa Zanzibar kuwashukuru kwa dhati Washirika wetu wa Maendeleo
kwa kuendelea kutuunga mkono, tunathamini mikopo, misaada na ushauri tulioupata
kutoka kwao”, alisema Dk. Shein.
Aidha,
Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa wakati unakaribishwa mwaka 2019 ni wajibu wa
kila Taasisi ya Serikali ikajipima namna inavyoendelea kutekeleza mambo
yaliyoagizwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015-2020.
“Nawakumbusha
viongozi wenzangu viongozi wenzangu wote wa CCM tuliochaguliwa na wananchi
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, uliorudiwa mwezi Machi, 2016. Kadhalika jukumu
hili wanapaswa walizingatie na wale wote niliowateua katika nyadhifa mbali
mbali”,alisema Dk. Shein katika risala yake hiyo.
Katika
risala yake hiyo Rais Dk. Shein alizitaja kumbukumbu za matukio yalitokea
katika mwaka 2018 ikiwa ni pamoja na utiaji wa saini wa Mkataba wa Mgawanyo wa
Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia (PSA), baina ya Kampuni ya Maendeleo ya
Mafuta na Gesi Asilia na kampuni ya RAK GAS ya Ras Al Khaimah.
Aliongeza
kuwa tukio jengine la kihistoria ni kufanyika kwa Tamasha la Utalii la
Kimataifa ambalo lilihudhuriwa na Makampuni 150 ya Utalii ya ndani na nje ya
nchi ambalo lilileta mafanikio katika kuwaunganisha wafanyabiashara wa utalii
wa Zanzibar na wale wa Kimataifa na kuitangaza Zanzibar katika masoko ya
Kimataifa.
Alieleza
kuwa mwaka 2018 umefungua milango katika utekelezaji wa dhamira ya kuendeleza
kilimo cha mpunga kwa njia ya umwagiliaji maji na utumiaji wa zana za kisasa ambapo
tarehe 6 Disemba, 2018 Serikali ilitiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa
Miundombinu ya Kilino cha Umwagiliaji maji na Kampuni ya Kokon Hansol JV ya
Jamhuri ya Korea kupitia Shirika la Maendeleo la nchi hiyo.
Pia,
Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika lengo la kuungana na nchi nyengine katika
kuendeleza uchumi wa Bahari tarehe 26 hadi 28 aliongoza Ujumbe wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika
mkutano wa Kimataifa uliofanyika Nairobi nchini Kenya.
Alisisitiza
kuwa kwa upande wa Zanzibar inauanza mwaka 2019
ikiwa imejipanga kwa kutafuta njia bora za kutumia rasilimali za bahari kwa
kuitumia vizuri bahari ya Hindi iliyoizunguka kwani hili ni eneo muhimu kwa
uchumi wa Zanzibar.
Akieleza
jambo jengine muhimu ambalo limefanyika katika mwaka 2018, Rais Dk. Shein
alisema kuwa tukio linalohusu jitihada za Serikali za kuwakinga wanawake wa
Zanzibar na janga la saratani ya shingo ya kizazi ambapo mnamo April 10 Mama
Mwanamwema Shein alizindua rasmi Mpango wa Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Saratani
ya Shingo wa Kizazi.
Vile
vile, tarehe 5 Disemba 2018 alizindua Mpango wa Miaka Minne wa Uchunguzi wa
Saratani ya Shingo ya Kizazi ambao unawajumuisha wanawake wenye umri wa miaka
21 hadi 65 kazi ambayo itafanywa kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Jamhuri
ya Watu wa China ambapo huduma zote pamoja na matibabu zitatolewa bure.
Rais
Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar inasifika kwa uzuri wake, historia yake na
khulka nzuri za watu wake na hali ya usalama iliyopo ambapo Serikali nayo
inafanya jitihada za kuhakikisha kwamba sifa njema ya Zanzibar ya kuwa ni
sehemu salama yenye utulivu inaendelea kwua ni kichocheo cha kuwavutia wageni,
watalii na wawekezaji sambamba na kurahisiha utekelezaji wa mipango ya
kamedneleo.
Hivyo,
mnamo tarehe 3 Novemba 2018 ulizinduliwa rasmi Mradi wa Ulinzi wa Mji
Salama ambao lengo lake ni kuhakikisha hali ya usalama kwa kutumia CCTV na
vyombo vyengine vya kisasa ambapo dhamira ni kuendeleza mradi huu katika Mikoa
mengine ya Unguja na Pemba hatua kwa hatua.
Licha
ya mafanikio hayo yaliopatikana mwaka 2018, Rais Dk. Shein alieleza kuwa bado
kunahitajika kuzidisha mapambano dhidi ya udhalilishaji wa wanwake na watoto na
unyanyasaji wa kijinsia kwa vile kesi za vitendo hivyo bado zinaendelea
kuripotiwa kwenye maeneo mbali mbali.
Sambamba
na hayo, Rais Dk. Shein aliwaahidi wananchi wote kwamba wale wote
watakaobainika kwamba wamehusika kwenye tukio la uvujaji wa mitihani ya kidato
cha Pili kwenye sekta ya elimu watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aliongeza
kuwa tukio hilo ni la kusikitisha, linalokwenda kinyume na mipango ya maendeleo
ya elimu ambalo halijengi mustakbali mwema wa elimu kwa watoto na kuwataka
wananchi kujifunza athari za tukio hilo kwa Serikali, Wizara, Walimu, Wazazi,
Wanafunzi na nchi kwa jumla.
Akimalizia
risala yake hiyo, Rais Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kushiriki kwa
wingi katika shughuli mbali mbali za kuadhimisha miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu
ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 zitakazofanyika katika maeneo yao kwani hizo ni
sherehe zao kila mmoja ahakikishe anashiriki ipasavyo katika hatua zote.