WAZIRI
wa Nishati Dk Merdad Kalemani ,wakati alipotembelea maonyesho ya bidhaa za
viwandani yanayoendelea viwanja vya sabasaba, Pichandege Kibaha Pwani, ikiwemo
banda la shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC), na kuelekeza kutangaza
vituo vinavyosambaza gesi asilia. (picha na Mwamvua Mwinyi)
.......................................................
NA MWAMVUA MWINYI, PICHANDEGE
WAZIRI wa Nishati Dk Merdad Kalemani ,amesema umeme ni injini ya
viwanda hivyo watahakikisha changamoto ya umeme kukatika kwenye viwanda nchini
inadhibitiwa kwani hali hiyo haifai viwandani .
Aidha amewataka wawekezaji waendelee kujenga viwanda kwani umeme uko wa
kutosha ambapo kwa sasa kuna akiba ya umeme wa ziada wa megawati 148.
Aliyasema hayo jana mjini Kibaha alipotembelea maonyesho ya viwanda
kwenye viwanja vya Sabasaba vilivyopo Picha ya Ndege wilayani Kibaha .
Hata hivyo aliielekeza TPDC kuvitangaza vituo vya gesi asilia ili
wananchi wapate uelewa juu ya gesi hiyo.
“Sera yetu kwa sasa tunataka sisi tutangulie na viwanda ndiyo viufuate na
siyo viwanda kuwafuata kwani kufanya hivyo tutakuwa tumewaondolea kero ya
kufuatailia masuala ya umeme,” alisema Dk. Kalemani.
“Ndiyo maana tunajenga miradi mikubwa ya uzalishaji umeme kama ule wa
Rufiji hydro power unaotokana na maji utakaozalisha megawati 2,100 na Rumakali
utakaozalisha megawati 358 na ule wa gesi wa Kinyerezi kuhakikisha viwanda
havikwami”
“Nimetembelea na kukagua mabanda na nimeona mahitaji na kati ya mabanda
17 ambayo ni ya viwanda wana sema umeme siyo tatizo licha ya sehemu kama
mbili wamelalamika kuwa umeme kwao ni changamoto”
Alibainisha wameona kuna mahitaji makubwa ya umeme kwa ajili ya
viwanda hasa katika maeneo ya Bagamoyo Kibaha na Chalinze viwanda vinajengwa kila
siku hivyo wilaya na Tanesco waainisheni maeneo ambako vitajengwa viwanda ili
miundombinu ipelekwe .
Aliwataka wataalamu wa Tanesco kuhakikisha wanaondoa changamoto ndogo
ndogo zilizopo .
Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama alisema watayaanisha
maeneo hayo ambayo yametengwa kwa ajili ya kuanzishwa viwanda ili huduma hiyo
ipelekwe kabla ya ujenzi wa viwanda kuanza.
Alisema wilaya yake ina viwanda vingi hivyo nishati ya umeme wa uhakika
ni muhimu kuwepo ili kuondokana na changamoto hizo za ukosefu au kukatika kwa
umeme.