Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani akiongea na wanahabari hawapo pichani wakati wa uzinduzi
wa mkutano wa siku moja wa wataalamu hao uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia
Sekta ya Mawasiliano Prof. Faustine Kamuzora akiongea na wataalam wa
Tehama wakati wa uzinduzi wa mkutano wa siku moja wa wataalamu hao uliofanyika
jijini Dar es Salaam leo.
Naibu Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani ameiagiza Tume ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano nchini kuhakikisha wanatengeneza misingi ya uadilifu wa
kitaaluma na misingi hiyo itumike kuwadhibiti wale ambao wanatumia utaalamu huo
kwa nia mbaya.
Mhandisi Ngonyani aliyasema hayo wakati
akizindua mkutano wa kwanza ambao umeandaliwa ma Tume mpya ya Teknolojia Habari
na Mawasiliano (TEHAMA) uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu
Nyerere jijini Dar es Salaam.
Alisema Mkutano huo una lengo la kuwakutanisha
wataalamu wa TEHAMA kutoka katika sekta za umma na sekta binafsi ili kuweza
kujadiliana ni kwa namna gani taaluma hiyo inavyoweza kutumika zaidi kwa faida
ya ukuaji wa uchumi nchini Tanzania.
“Wapo baadhi ya watu wanatumia taaluma ya
TEHAMA kwa manufaa mbalimbali ya kujenga uchumi na maendeleo, lakini wapo
wachache ambao wanatumia utaalamu wao kwa manufaa binafsi ikiwemo
kuwadhalilisha watu wengine na kuwaibia fedha zao katika mitandao” Alisema
Mhandisi Ngonyani.
Alisema Tume hiyo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano inatakiwa kuja na sheria kali ambazo zitawabana wale
wote ambao wamekua na tabia ya kutumia mitandao katika kufanya vitendo viovu
badala ya kutumia katika kujiletea maendeleo.
Awali akizungumza katika mkutano huo,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano upande wa sekta ya
Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora alisema uanzishwaji wa Tume ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano nchini ni jitihada za makusudi za serikali
katika kukuza Mawasiliano .
Prof,Kamuzora alisema kuwa tume hiyo ina
mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa na hivyo kuwasihi watendaji hao
kuwaelimisha zaidi wananchi kujikita zaidi katika kufuata maadili ya taaluma
hiyo ili kulifikisha Taifa katika mafanikio ya sekta ya mawasiliano.
Alisema Tume ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano itasaidia kukuza uchumi wa Taifa kutokana na kukua kwa sekta ya
TEHAMA na kuchochea uzalishaji ,ukuaji wa sekta zingine kiuchumi na usambazaji
wa huduma za jamii.
No comments:
Post a Comment