Tunapenda kutoa maelezo kutokana na taarifa
iliyotolewa katika gazeti la Jamhuri la Jumanne tarehe 16 – 22, 2016. Toleo na.
255 iliyokuwa na kichwa cha habari Prof. Muhongo avurunda.
Watanzania na Taifa kwa jumla wanashuhudia
jinsi Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Muhongo na viongozi wengine wote
wa Wizara ya Nishati na Madini wanavyofuatilia majukumu yao kwa karibu ikiwemo
sekta ya mafuta. Mhe. Prof. Muhongo na viongozi wa Wizara wamekuwa wakitoa
miongozo na maelekezo juu ya sekta ya mafuta ambapo kumeendelea kuwa na uhakika
wa upatikanaji wa mafuta nchini kwa wakati wote. Ni imani yetu kuwa Mhe. Prof.
Muhongo ataendelea kutekeleza majukumu yake vizuri na hivyo kuendelea kutimiza
matumaini ya Mhe. Rais na Taifa kwa jumla katika mambo yote yanayohusu wizara
ya nishati na madini ikiwemo sekta ya mafuta.
Tunapenda pia kueleza kuwa maagizo yote
aliyotoa kuhusiana na mafuta ya ndege yaliyokuwa yamechanganyika na mafuta ya
petroli yalitekelezwa kwa ukamilifu. Maagizo hayo yalikuwa ni Kampuni ya Sahara
kuondoa mafuta yaliyochanganyika kutoka katika maghala na mabomba na pia
kusafisha maghala na mabomba hayo ili kuwezesha kupokea mafuta mengine safi.
Kampuni ya Sahara ilitekeleza kwa ukamilifu maagizo haya. Usimamizi wa maagizo
haya ulikuwa kwa PBPA na EWURA ambapo taasisi hizi zilisimamia utekelezaji
wake. Hivyo si kweli kwamba Prof. Muhongo ameshindwa kusimamia maagizo yake.
Zuio la Kampuni ya Sahara kushiriki katika
zabuni lilitolewa na PBPA kwa kutumia mamlaka yaliyo katika Kanuni. Zuio hili
lilitolewa na PBPA ili kuhakikisha mafuta yaliyochanganyika yanaondolewa katika
maghala na kusafishwa kwa maghala hayo na mabomba ikiwa ni pamoja na
kukamilishwa kwa uchunguzi ili kutambua kuwa mafuta haya yalichanganyika sehemu
gani. Ifahamike kuwa mara baada ya meli iliyokuwa imeleta mafuta haya (mafuta
ya ndege na mafuta ya petroli) kufika hapa, mafuta hayo yalipimwa na TBS.
TBS walithibitisha kuwa mafuta yote katika
meli hii yako katika kiwango cha ubora unaotakiwa. Aidha, TBS walitoa idhini ya
kuteremshwa kwa mafuta hayo. Meli ilianza kuteremsha mafuta haya tarehe
4/5/2016 na kumaliza kuteremsha tarehe 8/5/2016. Meli hii iliruhusiwa kuondoka
mara baada ya kumaliza kupakua mafuta na taratibu zote kukamilika. Taarifa ya kuchanganyika
kwa mafuta haya ilitolewa tarehe 12/5/2016 wakati meli tayari ilikuwa
imekwishaondoka. Hivyo kulazimu kufanyika uchunguzi wa kujua ni wapi mafuta
haya yalichanganyika.
Suala la uchunguzi wa wapi mafuta
yalichanganyika lilikataliwa na makampuni ya mafuta kama ilivyokuwa
imependekezwa na kampuni ya Sahara. Makampuni ya mafuta yalisimamia katika
taarifa ya uchunguzi ya awali iliyofanywa na pande zote husika. Taarifa hii
ilikuwa na mapendekezo tofauti kati ya makampuni ya mafuta na kampuni ya Sahara.
Hivyo, kwa kuzingatia hatua hii kilichokuwa kimebakia ni kufuata mkataba kati
ya pande mbili hizi.
Kuondolewa zuio la Kampuni ya Sahara kushiriki
katika zabuni kulitolewa pia na PBPA kwa kutumia mamlaka yaliyo katika Kanuni.
Hii ilikuwa ni baada ya kuhakikisha kuwa mafuta yaliyochanganyika yameondolewa,
usafi wa maghala na mabomba umefanyika na kampuni ya Sahara imelipa thamani ya
mafuta yote yaliyoondolewa katika maghala.
Sheria ya Petroli (Petroleum Act, No. 21) ya
mwaka 2015 imetoa adhabu kwa yule atayaleta mafuta ambayo hayakidhi viwango vya
vya ubora unaotakiwa. Aidha, Kanuni ya uagizaji wa mafuta kwa pamoja (The
Petroleum (Bulk Procurement) Regulations) ya mwaka 2015 nayo imetoa adhabu juu
ya kosa la kuleta mafuta yasiyokidhi viwango vya ubora. Kutokana na mazingira
haya ya adhabu katika kosa tajwa, PBPA iliomba kupata mwongozo kutoka katika
Mamlaka za kisheria ili kuhakikisha kuwa adhabu inayotolewa iko katika misingi
sahihi ya ki-sheria.
Ni vyema ikafahamika kuwa hakuna sehemu ambapo
PBPA imedanganya Taifa. Ni kweli kabisa kuwa Sheria, Kanuni na Mikataba
inaeleza juu ya mafuta yaliyoletwa na kukutwa hayajafikia viwango vya ubora
unaotakiwa. Mafuta haya hayateremshwi na hutakiwa kurudishwa na yule
aliyeyaleta, ikiwa ni pamoja na kutekelezwa kwa taratibu zingine kwa mujibu wa
Sheria, Kanuni na Mkataba. Lakini, Sheria, Kanuni na Mkataba havina sehemu
inayoeleza juu ya mafuta yaliyofika, yakapimwa na kuthibitika kuwa yako katika
viwango vya ubora unaotakiwa, yakaruhusiwa kuteremshwa, meli ikaoondoka na
baadae kutambulika kuwa mafuta yaliyo katika maghala yamechanganyika.
Suala la ubora wa meli hushughulikiwa na TPA.
Taarifa za meli inayotakiwa kuleta mafuta hutumwa TPA ambao huthibitisha kama
meli hiyo inaruhusiwa au hairuhusiwi kuingia katika bandari zetu zinazotumika
kuteremsha mafuta.
Hitimisho, ni vyema ikafahamika kuwa utaratibu
wa uagizaji mafuta kwa pamoja hapa nchini umeanza tangu 2011. Utaratibu huu
umekuwa na mafanikio makubwa, hasa ikizingatiwa kuwa umejengwa katika misingi
ya uwazi na ushirikishwaji. Nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikifika kujifunza
kwetu. Aidha, hata taasisi zingine ndani ya nchi yetu ziko katika kutekeleza
manunuzi yao kwa kutumia utaratibu unaotumiwa na PBPA. Hii ni baada ya
kujifunza kutoka PBPA. Hii inaonesha ni kwa kiasi gani wadau mbali mbali
wanaona mafanikio ya utaratibu huu.
PBPA inapenda kuufahamisha umma kuwa
itaendelea kusimamia uagizaji wa mafuta kwa pamoja kwa kufuata Sheria, Kanuni
na Taratibu. Shughuli hizi zitafanywa kwa uwazi zaidi na kushirikisha wadau
wote wanaohusika. Tutabuni njia mbali mbali ili kuwezesha makampuni ya
Watanzania kuweza kushiriki katika biashara ya mafuta. Tunaamini kuwa tutaungwa
mkono na watu wote ili kuleta maendeleo ya nchi yetu.
Imetolewa na
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA)
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment