Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akipokea taarifa ya maendeleo ya
ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Dodoma kutoka kwa Eng. Guo
Zhingjian wa kampuni ya Chicco inayojenga kiwanja hicho, Mkoani Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa vitendo wakati alipokagua maendeleo ya ukarabati na upanuzi wa
kiwanja cha ndege cha Dodoma.
......................................................................................
Upanuzi na
ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Dodoma utakamilika mwishoni mwa mwezi Agosti
ili kuruhusu ndege za abiria sabini mpaka tisini kuweza kutua na kuruka na
hivyo kurahisisha usafiri wa anga kwa ukanda wa kati.
Hayo yamesemwa na Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa baada ya kutembelea
kiwanjani hapo kukagua hatua ya mwisho ya ujenzi iliyofikiwa ambapo amesema
kasi ya Mkandarasi Chicco anayetekeleza kazi hiyo inaridhisha katika
kuhakikisha kiwanja hicho kinakamilika kwa muda na kwa viwango
vilivyokubalika.
Amesema mpaka sasa ni
asilimia themanini ya kazi iliyotekelezwa kwa siku arobaini na tano tangia
kuanza ukarabati hivyo kasi iliyotumika kwenye kiwanja hiki itatumika kwenye
ujenzi wa viwanja vingine nchini.
“Tunaamini kabisa kwa
kasi ya mkandarasi na msimamizi mtakamilisha ujenzi huu haraka na viwango
tulivyokubaliana katika mkataba ili ndege kubwa zianze kutua na kuruka” amesema
Prof. Mbarawa. Naye Msimamizi wa ujenzi wa kiwanja hicho kutoka Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Eng. Mhandisi Mbila Mdemu amesema kazi ya
ukarabati na upanuzi inaendelea kufanywa usiku na mchana kwa kuzingatia ubora
na viwango na kukamilika kwa wakati
“Tulipewa kazi hii na
tunaahidi kuwa itakamilika kama tulivyoelekezwa ili kuwapa wananchi
wanaozunguka mikoa ya Dodoma na jirani fursa ya kutumia usafiri wa Anga”,
amesema Eng. Mdemu. Ameongeza kuwa kazi zinazokamilishwa sasa ni kumalizia
sehemu ya maegesho ya ndege na tabaka la mwisho kwenye barabara ya kuruka na
kutua ndege.
Mradi wa upanuzi na
ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Dodoma umegharamiwa na Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa zaidi ya shilingi bilioni 11.8 na kukamilika kwake
kutaongeza idadi ya safari za ndege zitakazosafirisha abiria wa mikoa ya kanda
ya kati.
No comments:
Post a Comment