Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akitoa taarifa rasmi ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa Zanzibar wa awamu ya pili Mzee
Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea leo Mji Mwema Dar es Salaam na kuzikwa kesho
katika viwanja vya nyumbani kwake Migombani Unguja.[Picha na Ikulu.]15/08/2016.
………………………………………………………………………………….
Kwa masikitiko makubwa, naomba
kuwaarifu kuwa, leo tarehe 14 Agosti 2016, Mzee wetu Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi
amefariki dunia.
Kama mnavyofahamu, Marehemu Mzee Aboud Jumbe ni Rais Mstaafu
wa Zanzibar awamu ya pili, ambaye vile vile alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Marehemu Mzee Aboud Jumbe amefariki dunia baada
ya kuugua kwa muda mrefu kutokana na umri wake.
Msiba huu umetokea nyumbani kwake Mji
Mwema, Dar es salaam. Maziko ya marehemu yatafanyika kesho tarehe 15 Agosti
2016 saa 7.00 mchana ambapo maiti yake itasaliwa katika Masjid Mshawar,
Mwembeshauri na kuzikwa nyumbani kwake Migombani.
Kufuatia mchango na juhudi
mkubwa ambazo marehemu Mheshimiwa Aboud Jumbe Mwinyi alizichukua katika uhai
wake kwa kuitumikia, kuiongoza na kuijenga Zanzibar pamoja na nafasi yake
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi yetu imekabiliwa na msiba mkubwa
kwa kifo cha kiongozi huyu mahiri.
Kutokana na msiba huu mkubwa kwa nchi
yetu, natangaza rasmi siku saba za maombolezo, kuanzia kesho tarehe 15 Agosti
2016.
Katika kipindi hicho chote bendera zote zitapepea nusu
mlingoti. Kadhalika utaratibu wa maziko utafuata wasia ambao mwenyewe
marehemu aliutoa wakati wa uhai wake.
Tunaungana na wanafamilia wote katika
kipindi hiki kigumu cha msiba. Naomba kutumia nafasi hii kutoa mkono wa
pole kwa wafiwa wote. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie kauli thabit
marehemu mzee wetu na amlaze pahala pema peponi, Amin.
Inalillahi wainnailaihi rajiun
No comments:
Post a Comment