Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza tabia kwa baadhi ya watu wakiwemo wasanii watu wengine mmoja mmoja
kutumia mavazi yanayofanana na sare za Majeshi ya Ulinzi na usalama hapa nchini
likiwemo Jeshi la Polisi katika shughuli zao za kisanii au katika kazi mbalimbali,
Jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za Nchi.
Kwa mujibu wa Sheria ya
kanuni za makosa ya Jinai, sura ya 16 na marejeo yake ya mwaka
2002, kifungu cha 178 (1) na (2) kinachozungumzia makosa dhidi ya
sare za majeshi ya ulinzi na usalama, kinabainisha wazi kuwa ni kosa
kisheria kwa mtu yeyote ambaye siyo mtumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama
kuvaa mavazi yanayotumiwa au kushabihiana na sare za majeshi hayo bila
kibali kutoka kwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufuatia kitendo kilichofanywa na kundi la kisanii la “ Original
Comedy” kuvaa mavazi yanayoshabihiana na sare za Jeshi la Polisi, Jeshi la
Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam linachukua hatua za kisheria dhidi
ya wasanii hao.
Aidha Jeshi la Polisi nchini, linatoa onyo kali kwa mtu ama kikundi
chochote kuacha kutumia mavazi yanayofanana na sare zinazovaliwa na
majeshi ya ulinzi na usalama hapa nchini na atakayebainika hatutasita kuchukua
hatua kali za kisheria dhidi yake.
Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wale wote wenye mavazi yanayoshabihiana
na sare za majeshi ya ulinzi na usalama kuzisalimisha mara moja katika
vituo vya Polisi vilivyokaribu nao.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba – Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
No comments:
Post a Comment