Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akifafanua jambo kwa waandishi wa
habari (hawako pichani) kuhusu utekelezaji wa agizo la kuondoa watumishi hewa
katika orodha ya malipo ya mishahara Serikalini ofisini kwake mapema leo.
..............................................................................................
Waajiri 264 kati ya waajiri wote 409 Serikalini wamewasilisha taarifa zao
kuhusu kuwepo kwa watumishi hewa ambapo kati ya waajiri hao waajiri 63
wamethibitisha kwamba hawana watumishi hewa katika Taasisi zao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Angellah Kairuki (MB), amebainisha hayo wakati alipozungumzia na
waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa waajiri
201 wana watumishi hewa kuanzia mmoja na kuendelea.
“Waajiri 264 kati ya waajiri wote 409 wamewasilisha taarifa zao kuhusu
uwepo wa watumishi hewa. Kati ya waajiri 264 waliowasilisha taarifa zao,
waajiri 63 wamethibitisha kwamba hawana watumishi hewa katika Taasisi zao na
waajiri 201 wana watumishi hewa mmoja (1) na kuendelea.” Alisema Waziri
Kairuki.
Hata hivyo, alisema zipo taasisi 145 ambazo hazijawasilisha taarifa iwapo
zina watumishi hewa au la ikiwemo Mabaraza 11, Bodi 10, Vyuo Vikuu 25,
Hospitali 3 na Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa 12.
Alizitaja taasisi nyingine kuwa ni Mamlaka 6, Tume 10, Mamlaka za
Serikali za Mitaa 38, Taasisi za
Umma na Wakala 30 ambapo aliziagiza Taasisi zote ambazo hazijawasilisha taarifa
za watumishi hewa kufanya hivyo kabla au ifikapo tarehe 26 Agosti mwaka huu.
Waziri Kairuki alieleza kuwa kuanzia Agosti 15 mwaka huu, ofisi yake
ilianza zoezi la uhakiki wa kushtukiza katika taasisi sabini za Serikali
zikiwepo Wizara, Idara za Serikali Zinazojitegemea na kwamba zoezi hilo
linaendelea.
Aliongeza kuwa uhakiki wa kustukiza utafanyika pia kwenye Sekretarieti za
Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma kwa madhumuni ya
kujiridhisha kwamba taarifa za watumishi hewa zilizowasilishwa na waajiri ni
sahihi.
Alibainisha kuwa katika kufanikisha uhakiki
huo, Ofisi yake imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuendelea kutoa mafunzo ya mara
kwa mara kwa Maafisa Utumishi wenye dhamana ya kutumia mfumo wa malipo ya
mshahara kukuza uwajibikaji kwa maafisa wanaosimamia malipo ya mishahara kwa
kuwachukulia hatua za kinidhamu au kisheria wanaobainika kusababisha watumishi
hewa.
“Aidha ofisi yangu pia inafanya
uhakiki wa kushtukiza na kuanza safari ya kuunganisha Mfumo wa Malipo ya
Mishahara na mifumo mingine mikubwa kama ya NIDA, RITA na Baraza la Mitihani la
Taifa, na kuwezesha mfumo kuwaondoa moja kwa moja (automatically) watumishi
waliofikisha umri wa kustaafu kwa lazima.” alisema.
Waziri Kairuki atatoa taarifa kamili ya watumishi hewa baada ya kupata
taarifa hizo kutoka kwa waajiri ambao hawajawasilisha taarifa hizo na
kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa Taasisi sabini (70) linaloendelea sasa.
“Hivyo naagiza Taasisi zote
ambazo hazijawasilisha Taarifa za Watumishi Hewa kufanya hivyo kabla au ifikapo
tarehe 26 Agosti, 2016.” Alisema Waziri Kairuki.
Alisema kuwa ofisi yake itawasilisha taarifa rasmi ya watumishi hewa kwa
Mheshimiwa Rais ikiwa na orodha na majina ya Taasisi ambazo zimewasilisha
taarifa ya watumishi hewa na na zile ambazo hazijawasilisha taarifa hizo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mnamo
Machi 15 mwaka huu aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Waajiri wote kwa ujumla
kuchukua hatua ya kuhakikisha katika Mikoa au Taasisi zao hakuna watumishi hewa
ifikapo tarehe 30 Machi, 2016.
Katika kutekeleza agizo hilo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa agizo hilo na
mnamo Mei 26 mwaka huu waajiri wote waliagizwa kuwasilisha taarifa za
mwisho za zoezi la kuwabaini na kuwaondoa watumishi hewa katika orodha za
malipo ya mshahara (payroll) ifikapo mwisho wa Mwezi Juni, 2016.
Waajiri walitakiwa kutuma jina la Taasisi, Fungu la Taasisi (Vote), namba
ya Utambulisho ya Mtumishi wa Umma (Cheki Namba), jina kamili la mtumishi; cheo
cha mtumishi, jina la tawi la Benki ambalo mshahara wa mtumishi umekuwa
ukipitishwa au ukilipwa.
Taarifa nyingine zinazotakiwa kutumwa ni hatua zilizochukuliwa na mwajiri
dhidi ya watumishi hewa waliobainika kama kurejesha fedha, na Maafisa wengine
wa Taasisi husika waliosababisha uwepo wa Watumishi hao kuwachukulia wahusika
hatua za kinidhamu au kisheria.
Nyingine ni namba ya akaunti ya Benki ya mtumishi, tarehe ambayo mtumishi
aliondolewa kwenye mfumo wa taarifa ya Kiutumishi na Mshahara, kiasi cha fedha
zilizolipwa kwa mtumishi husika tangu alipotakiwa kuondolewa hadi tarehe
aliyoondolewa kwenye mfumo na sababu ya kuondolewa kama utoro, kufariki dunia,
kuacha kazi, kustaafu na sababu nyingine.
No comments:
Post a Comment