Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi
Kitongoji hapa nchini kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa
ajili ya kutoa elimu bila malipo kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi
mabaya ya fedha hizo.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe
01 Agosti, 2016 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani
na kuwajumuisha wananchi wa Katoro na Buseresere Mkoani Geita.Katika agizo hilo
Dkt. Magufuli amewaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa
kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi kwa lengo la kupata
mgao mkubwa wa fedha za ruzuku na amesema Serikali itachukua hatua kali dhidi
ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
"Ninafahamu mgao wa fedha hizo hutolewa
kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo, wapo baadhi ya walimu ambao wameanza
kuandika wanafunzi hewa katika shule zao, ili kusudi aletewe hela nyingi kuliko
idadi ya wanafunzi waliopo, wanafunzi kama wapo laki nne yeye anasema shule
yangu hii ina wanafunzi laki tano, ili kusudi hela zikija za wanafunzi laki
tano, za wanafunzi laki moja wagawane."Napenda nitoe wito kwa walimu
Tanzania nzima, mnatafuta matatizo, narudia mnatafuta matatizo, msijaribu kula
hela ya Serikali" Amesema Rais Magufuli.
Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli pia
ametaka viongozi wa ngazi zote katika Mikoa kuhakikisha wana takwimu za idadi
ya wanafunzi katika shule zote zilizopo katika maeneo yao ili kurahisisha
ufuatiliaji wa fedha hizo na amesema kuwa kuanzia sasa ataanza kutembelea shule
kwa kushitukiza na kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua takwimu itakuwa ni
uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa alionao.
"Na nitoe wito kwa viongozi wa Mikoa,
Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tarafa, Watendaji wa Kata,
Wenyeviti wa Vijiji, kila mmoja awe na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule
zao, hatutaki kuwapunja wanafunzi hela ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia
hatutaki kutoa hela ambayo haitakiwi" Amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ametumia mkutano huo
kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali yake ya Awamu ya Tano,
kutekeleza ahadi yake ya kujenga Tanzania Mpya pia amewataka viongozi na
watendaji wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea wananchi
wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi ofisini huku akisisitiza ofisi hizo
kuwepo katika maeneo yenye shughuli husika.
Aidha, Dkt. Magufuli amekosoa utaratibu
unaotumiwa na Halmashauri nyingi za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kutumia
mawakala katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri akisema mawakala hao
wamekuwa wakitumia utaratibu huo kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha
kiasi kidogo katika Halmashauri husika.
"Hivi kwa nini Halmashauri msingekuwa na
maafisa wenu wazuri na mkawa na mashine za kielektroni kwa ajili ya kukusanya
fedha? Amehoji Dkt. Magufuli na kuongeza kuwa "tena mawakala wengine ndio
hao hao wamekuwa wakikusanya kodi hata kwa wananchi wanyonge wenye vibiashara
vidogo vya kuuza mchicha bila hata kuwaonea huruma"
Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama
Janeth Magufuli amemaliza ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida,
Tabora, Shinyanga na Geita na yupo nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa
mapumziko mafupi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
01 Agosti, 2016
No comments:
Post a Comment