Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Msanii wa muziki
wa taarab Bi. Shakila Said kilichotokea ghafla nyumbani kwao Mbagala jijini Dar
es Salaam jana Ijumaa ya tarehe 19/08/2016.
Shakila ni msanii na mdau
wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa na mchango mkubwa katika kukuza
muziki wa taarab nchini hasa katika kubuni kazi za Sanaa za muziki mbalimbali
ambazo zilikuja kupata umaarufu mkubwa. Moja ya kazi alizobuni na kupata
umaarufu mkubwa ni pamoja na 'Macho yanacheka' na 'kifo cha mahaba'.
Mchango wake katika
muziki wa taarab hasa katika kubuni na kutunga nyimbo zenye ubora, ujumbe na
maadili kwa jamii hautasahaulika kamwe. Ni mwanamuziki aliyeacha misingi katika
sekta ya muziki na alijitolea kwa kiasi kikubwa katika kuufikisha muziki wa
taarab mahali ulipo leo.
Baraza, wasanii na wadau
wote wa Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote aliyotuachia marehemu
Shakila hasa katika kupenda kujitolea muda mwingi katika kukuza muziki wa
taarab na sekta ya muziki kwa ujumla.
Baraza linatoa pole kwa
ndugu wa marehemu, shirikisho la muziki, wasanii na wadau wote wa Sanaa katika
kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu.
No comments:
Post a Comment