Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako
ametoa siku saba kuanzia Agosti 17, 2016 kwa vyuo vikuu kurejesha fedha
zilizopokea ambazo ni za wanafunzi ambao hawapo chuoni.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam alipokuwa
akiongea na waandishi wa habari juu ya taarifa la zoezi la uhakiki wa wanafunzi
wanufaika wa mikopo vyuo vya Elimu juu.
Prof. Ndalichako amesema kuwa uhakiki wa wanafunzi hao umefanyika
katika vyuo 31 kati ya vyuo 81 vilivyopo nchini, Katika utafiti huo wanafunzi
2,192 wameshindwa kuhakiki majina yao, hivyo kushindwa kuthibitisha uwepo na
uhalali wa wanafunzi hao.
“Mikopo ya Wanafunzi hao imesitishwa na kwa wale ambao ni wanafunzi
halali lakini walishindwa kujihakiki itabidi waombe tena mkopo,” alifafanua
Mhe. Ndalichako.
Ameendelea kwa kusema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2015/16 wanafunzi hao hewa
wameigharimu Serikali kiasi cha shilingi 3,857,754,460, kiasi ambacho
kinatakiwa kurejeshwa na vyuo ambavyo wanafunzi hao wamebainika.
Aidha, Prof. Ndalichako amesema kuwa taarifa hiyo imekabidhiwa
kwenye vyombo vya sheria ili kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika
kufanya udanganyifu na kusababisha Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.
Vile vile Prof. Ndalichako amewataka wakuu wa vyuo kuweka mfumo wa
kuhakiki usahihi wa matokeo ya wanafunzi yanayotumwa Bodi ya Mikopo
kutokana na vyuo vingi kubainika kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwenye matokeo
ya wanafunzi ambao hawakufanya mtihani au waliofeli na kuandikiwa wamefaulu ili
waendelee kupata mikopo.
No comments:
Post a Comment