Sunday, August 21, 2016

MGOGORO KATI YA WAFUGAJI NA WAKULIMA BAGAMOYO, RC AINGILIA KATI.

mas3
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza na kundi la  wafugaji ,huko Kitomondo kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo, akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na Usalama mkoani humo ili kurejesha amani katika eneo hilo baina ya wafugaji na wakulima (Picha na Mwamvua Mwinyi)
 mas1

Mfugaji huko Kitomondo, kata ya Makurunge, wilayani Bagamoyo ,Gidufana Gafufen akitoa kero za wafugaji kwenye kata hiyo kwa mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo, aliyefika katika eneo hilo kurejesha amani baada ya kutokea  mgogoro baina ya wakulima  na wafugaji (Picha na Mwamvua Mwinyi)
 mas2

Wafugaji huko Kitomondo kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo, wakimlilia mwenzao Gegona Mulamu(25) aliyefariki dunia baada ya kutokea  mgogoro baina yao na wakulima .
.............................................................................................................


Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo

KAMATI ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, imeingilia kati mgogoro baina ya wakulima na wafugaji katika  kijiji cha Kitomondo ,kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo baada ,mgogoro huo kusababisha kifo cha mfugaji Gegona Mulamu (25) na mkulima aliyejulikana kwa jina la Daudi kujeruhiwa.

Hatua hiyo imemlazimu mwenyekiti wa kamati hiyo ,mhandisi Evarist Ndikilo, kuunda kamati ya uchunguzi itakayofanya kazi kwa siku 14  ili kuchunguza tatizo la mgogoro huo.

Amesema katika kamati hiyo atakuwepo mjumbe kutoka kwa wakulima mmoja na mfugaji  ambao watawasilisha mambo yote yaliyotokea na kero zinazowakabili, mjumbe ofisi ya mkuu wa mkoa anaeshughulika na masuala ya mifugo na kilimo.

Mhandisi Ndikilo ametaja wengine ni kutoka ofisi ya mkuu wa usalama mkoa, ofisi ya taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) na mjumbe kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali.

Chanzo cha mgogoro huo inaelezwa ni baada ya wafugaji kudaiwa kuingiza mifugo yao katika baadhi ya mashamba ya wakulima na kusababisha mazao yote kuliwa hivyo wakulima kupata hasara.

Hata hivyo wafugaji hao walisusia kusuluhishwa na kuzungumza na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Bagamoyo, kwa kudai kuwa hawana imani na kamati hiyo.

Baada ya mkuu wa mkoa kufikishiwa taarifa hiyo ,aliamua kuambatana na kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapo kwenda eneo la tukio ili kurejesha amani.

Mhandisi Ndikilo alifika katika eneo hilo majira ya saa 11 jioni ,agost 20 na kamati hiyo ambapo walikuta wakulima peke yao katika mkutano wa hadhara uliolenga kupatanisha pande hizo huku wafugaji wakiwa wamesusia.

Mkuu huyo wa mkoa aliomba msafara uende hadi eneo walipo wafugaji ,ambako ni kwenye vichaka ambapo waliweka kambi kwa siku nne kumlilia mwenzao ambae inasadikiwa alipigwa risasi na polisi ambae alienda kuwatishia.

Mhandisi Ndikilo alieleza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria hivyo yeyote atakaebainika kusababisha kifo cha mfugaji Gegona Mulamu (25)  atachukuliwa hatua.

Aliomba amani iwepo katika eneo hilo na kuwaomba wakulima na wafugaji washirikiane na kuondoa tofauti zao ili kupisha serikali ishughulikie tatizo hilo.

Alizitaka pande hizo kuheshimiana, kushirikiana bila kutishiana na ambae atajaribu kumtishia mwenzie serikali haiwezi kumvumilia.

Kwa upande wa wafugaji hao akiwemo Lucas Kinan ,aliiomba serikali ya wilaya kusimamia hakibadala ya kuegemea upande mmoja wa  wakulima.

Alisema wanataka uchunguzi ufanyike kujua aliyemuuwa mwenzao ili sheria ichukue mkondo na pia kujua ni namna gani familia ya marehemu itaishi.

“Baadhi yetu tunajua aliyesababisha kifo ni polisi kwani hapa sisi hatuishi na risasi na tumeokota ganda la risasi. ambapo siku ya tukio polisi walikuja na kutuondosha Gedona Mulamu amabe ni marehemu alikaidi ndipo alipopigwa “alisema Kinan.

Kinan alisema hawana haki mbele ya wakulima na baadhi ya viongozi wamekuwa sehemu ya mashamba ya wakulima.

Alieleza kuwa hawajawahi kufikia hatua ya  mgogoro wakufikia kuuwana ama kujeruhiana lakini kwasasa yanaibuka hayo kutokana na baadhi ya viongozi kutumia mikutano kuleta agenda za kugombanisha wakulima na wafugaji badala ya kusimamia haki.
 
Nae Gidufana Gafufen, alisema baadhi ya watendaji wa vijiji, kata wanapendelea wakulima na kunyanyasa wafugaji na halmashauri  iliamuru wafugaji wote waondoke ama wafuge kwa kuwafungia ng’ombe zao ndani na sio malishoni.

Kwa upande wa wakulima kwenye eneo hilo walisema hawana amani na uwepo wa wafugaji hao kutokana na kutishiwa kwa kupigwa mishale na mazao yao kumalizwa na mifugo.

Walimuomba waziri wa mifugo na kilimo kwenda kuwaweka meza moja ili kuangalia namna ya kuweka suluhu kwa matatizo yao.

No comments:

Post a Comment