MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani,mhandisi Evarist
Ndikilo,amesema wanaendelea na mapambano katika eneo la Vikindu na kuimarisha
ulinzi wilayani Mkuranga kufuatia kutokea matukio ya uvunjifu wa amani
yaliyotokea hivi karibuni.
Aidha amevitaka vyama vya siasa mkoani humo, kuacha kufanya
maandamano ikiwemo ya umoja wa kupinga udikteta(UKUTA)na chama kitakachobainika
hatua kali zitachukuliwa.
Katika hatua nyingine mhandisi Ndikilo ,amewaomba viongozi wa dini
wasichoke kuliombea taifa,kumuombea rais John Magufuli na viongozi wote ili
waendelee kuwatumikia wananchi kwa maslahi mapana ya taifa.
Aliyasema hayo, wakati kamati ya amani ya mkoa wa Pwani,ilipokwenda kutoa
pole kwa kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo, kutokana na matukio ya
kiuhalifu yaliyotokea wiki iliyopita wilayani Mkuranga.
Alisema kuwa serikali hiyo, imejipanga kikamilifu kulinda amani ya
wananchi na mali zao sambamba na kuimarisha ulinzi wilayani Mkuranga na maeneo
mengine ya mkoa huo.
“Tutahakikisha tunapambana na
suala hili kwa kushirikiana na jeshi la polisi Dar es salaam na kwa kupitia
uongozi wa amiri Jeshi mkuu litakwisha kwani amedhamiria kwa dhati kupambana na
jambo hili ,”
“Na askari hawajakatishwa tamaa
,licha ya kutokea kwa matukio hayo na kwasasa askari wengine bado wanaendelea
na mapambano katika maeneo ya wilaya hiyo ili kufichua wahalifu wengine” alisema mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo, alielezea kuwa, kuna kila sababu ya kuimarisha ulinzi na
usalama ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Alisema dhamana ya kulinda amani ya watanzania ni ya serikali iliyopo
madarakani na wakuu wa mikoa ni wasaidizi wa mh. Rais na wenyeviti wa kamati za
ulinzi na usalama hivyo atahakikisha anasimamia suala hilo.
Hata hivyo, mhandisi Ndikilo, aliitaka kamati ya amani mkoa, iendelee
kushirikiana na serikali ngazi ya wilaya na kuangalia namna ya kuunda kamati
hizo wilayani ili zishirikiane kuimarisha utulivu.
Akizunguzmzia kuhusiana na maandamano yanayotarajiwa kufanyika sept mosi
mwaka huu,na umoja wa kupinga udikteta(UKUTA),alisema mkoani humo
hayataruhusiwa.
Mhandisi Ndikilo,alieleza maandamano hayo hayana tija na mwisho wa siku
ni kuleta vurugu na kuhatarisha amani ya mkoa na nchi kijumla hivyo utii wa
sheria bila shuruti unahitajika.
Alisema ni vema vyama hivyo vikazingatia taratibu zilizowekwa na serikali
ili kuepusha uvunjifu wa amani katika mkoa na endapo kipo chama kitakachokaidi
taratibu zilizowekwa, hakitoweza kuvumiliwa.
Mhandisi Ndikilo,aliomba viongozi wa dini wayakataze kwa waumini wao
kupitia misikiti na makanisa kwani yamepigwa marufuku.
“Haijakatazwa mikutano ya siasa
bali wafanyie kwenye maeneo yao ya kazi kama ni mbunge ama diwani afanye kwenye
eneo lake,sio diwani wa mailmoja aende Chalinze hapana,mtusaidie kufikisha
salamu kuwa mkoa hautaki kusikia wala kuona maandamano ya UKUTA sijui nini” alisisitiza mkuu huyo.
Kwa upande wake ,kamanda wa polisi mkoani
Pwani, kamanda Boniventure Mushongi ,alitoa rai kwa jamii kuendelea kutoa
ushirikiano na jeshi la polisi kufichua wahalifu.
Alisema kwasasa wanaendelea na kulinda maeneo mbalimbali ya wilaya ya
Mkuranga na kusema matukio mbalimbali yanatokea mara kwa mara wilayani humo,
kutokana na maeneo mengi kuwa mapori ambapo baadhi ya watu wahalifu wamegeuza
kuwa choo na maficho yao.
Kamanda Mushongi ,alisema jeshi hilo halitosita kuingia kwenye mapori na
maficho ambayo wananchi wasamaria wema watatoa taarifa kwa polisi kuyafanyia
kazi.
Alisema kuwa ,kikulacho kinguoni mwako hivyo inapaswa jamii itambue hilo
kwa manufaa ya mkoa na taifa kijumla.
Kamanda Mushongi,alieleza wananchi wajaribu kuwa macho
ambapo aliwaomba watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kutoa mwiba
unaosumbua.
Aliasa amani ilindwe na kila mmoja na ni jukumu la kila mmoja kuwa mlinzi
wa mwingine na kushirikiana.
Katika kamati ya amani mkoani hapo,ina wenyeviti
wenza wawili,alhaj shekhe Hamis Mtupa na padre Beno Kakudo,ambao waliliomba
jeshi la polisi lisikatishwe tamaa na yaliyotokea.
Alhaj Mtupa alisema,kweli polisi wengine wamepoteza maisha lakini
wasikatishwe tamaa kwani polisi hao wamepotea maisha wakiwa kwenye mapambano na
majukumu yao ya kazi.
Alihakikisha kuwa kwa nafasi zao kama viongozi wa kiroho wapo pamoja na
wananchi na vyombo vya dola ambavyo vipo kwa ajili ya kulinda jamii na mali
zao.
Alhaj Mtupa alisema viongozi wa kisiasa wajaribu kujenga tabia ya kupenda
kukaa kwenye meza za mazungumzo ,kupatanisha na kujadili mambo kuliko kwenda
katika hatua za maandamano,migogoro ama mapambano hali ambayo inawaweka
wananchi katika hali ngumu.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama,alichukuwa fursa
hiyo,kukemea maandamano hayo na kusema atakaekiuka taratibu zilizowekwa na
serikali itageuka kichaka badala ya Ukuta.
Alisema Ukuta wanataka muafaka anashangaa hakuna tatizo ,watu wanafanya
fujo halafu hao hao wanasema wanataka muafaka.
Assumpter alisema,wapo watu wanafanya mambo kwa kutaka kuvuruga amani ya
nchi wakati nchi siyo ya kuichezea
Aliomba vijana na wananchi wilayani Kibaha,wawe watulivu siku ya sept
mosi ili kuondokana na madhara yanayoweza kujitokeza.
Mnamo agost 26 mwaka huu mapigano makali yalitokea baina ya askari polisi
na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi huko eneo la Vikindu wilayani Mkuranga
na kusababisha askari mmoja kufariki dunia na majambazi 14.
Agost 24 majira ya saa 1 /2 usiku ,uvamizi na shambulizi lenye nia ya
uovu lililofanywa na kundi la majambazi na kuwauwa askari wanne huko Mbande
huko Temeke,ambapo majambazi waliofanya tukio hilo wanadaiwa kuuwawa katika
tukio la agost 26 eneo la Vikindu.
No comments:
Post a Comment