Umoja wa
Vijana wa CCM tuliutangazia umma na dunia kwamba ifikapo Agosti
31 mwaka huu tutaitisha maandamano ya amani nchi nzima yenye lengo la kuunga
mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe
Magufuli kwa utendaji wenye tija, ufanisi na uliorudisha imani na matumaini kwa
wananchi.
Msimamo na
dhamira ya kufanya maandamano hayo ya amani yenye maudhui na kusudio hilo, bado
uko pale pale ingawaje si kwa tarehe tuliopanga na kutangaza awali yaani Agosti
31 mwaka huu.
Jumuiya
yetu kama mjuavyo ni ya Vijana wa CCM, (UVCCM) inapata malezi kwa karibu mno na
Jumuiya ya Wazazi ya CCM. Wiki ya jana Mwenyekiti wa Wazazi Taifa Nd. Abdallah
Bulembo alikutana na waandishi wa habari akitutaka UVCCM tuahirishe
maandamano ya Agosti 31 mwaka huu hadi wakati mwingine.
Kwa mujibu
wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, Jumuiya ya Wazazi ndiyo Msimamizi wa Malezi,
Maadili na Adabu kwa Vijana wote nchini, sisi UVCCM tunaamini kuwa sikio
halishindani na kichwa, mtoto ni mtoto kwa Wazazi wake hakui, hana jeuri wala
ubishi.
Mtoto au
watoto wanaokaidi amri, ushauri au maelekezo ya Wazazi wao huitwa watukutu,
wenye viburi, manunda na wasioambilika. UVCCM si watukutu, hatukufunzwa
tuwe wabishi, wakaidi na wenye viburi.
Tumezingatia kutii maelekezo,
makatazo na maonyo , tumeambiwa tuahirishe maandamano yetu nasi tumekubali na
kuheshimu mambo tuliyoaswa.
Sambamba na
hilo tumepata majibu ya barua yetu tuliyomwandikia Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini (IGP Ernes Mangu) inayotutaka tuache kufanya maandamano yetu kwa sababu
Polisi wamezuia mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa na maandamano nchi
nzima.
Jambo
jingine ambalo limetufanya pia tuahirishe maandamano yetu ya Amani ni taarifa
ya kintelejinsia iliowasilishwa na Kamati yetu ya Usalama na Maadili ya UVCCM
mbele ya kikao cha Sekreteriet yetu, nayo ilipendekeza suala hilo
liahirishwe kwa wakati huu hadi muda mwingine.
Pia jambo
jingine ambalo limefanya maandamano hayo tuyabatilishe ni kulipisha Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) ambalo litakuwa katika shughuli za maadhimisho
miaka 52 tokea kuanzishwa kwake.
Wanajeshi
wetu watakuwa katika kazi mbalimbali za kijeshi kwenye kambi zao na mitaani
kufanya usafi wa mazingira, hivyo isingependeza na wala si heshima wakati sisi
tukiandamana, wao wakifanya kazi muhimu kila mmoja wetu zinazomgusa badala yake
ni vyema kuwaunga mkono jambo wanalolifanya la usafi wa mazingira.
UVCCM
tumekubali, hatutaki kuingia katika uvunjaji wa sheria hasa baaada ya kutakiwa
kuahirisha na mamlaka za Kisheria hadi wakati mwingine muafaka na si wakati
huu.
Tunaelewa
kwamba uamuzi wetu wa awali wa kutaka kuandamana kwa amani hata kama
tungenyimwa kibali ungetugharimu, ungetusababishia madhara na pengine hasara,
kwa wakati huu na kuona jambo lenyewe ni la kuipa Ari serikali katika kuhimiza
Uwajibikaji, Utendaji na Usimamizi bora wa Uendeshaji wa masuala ya kiutawala.
Tulishusha
maagizo kwa Makatibu wetu wote wa Mikoa yote 32 na Wilaya 171 ya Kichama
tukiwataka waandike barua katika Ofisi za Ma RPC na OCD, washirikiane ili
kuratibu maandamano na kuyafanikisha kama tulivyokusudia.
Watendaji
wetu wa ngazi husika wamefuata maelekezo, wametii taratibu zetu za kiutendaji
na leo tumewajulisha tena wasitishe maandamano hadi tutakapowapa tena maelekezo
mengine. Tunawahimiza na kuwataka ni vyema kutii mamlaka za Kikanuni na
Kisheria.
UVCCM kwa
wakati huu tumeamua kuachana na maandamano badala yake tunajikita katika
matayarisho ya kuwapeleka Vijana wetu wakashiriki katika Mafunzo ya Siasa,
Utawala, Uongozi, Ufundi na Ujasiriamali yatakayoanza kufanyika katika Chuo
chetu kilichopo huko Ihemi Mkoani Iringa ambapo kitakuwa kielelezo na alama
nzuri ya kumuunga mkono Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa vitendo.
Tumewataka
Makatibu wetu wa Mikoa na Wilaya kuendelea na zoezi la Uratibu na Uhakiki
kwa Vijana ambao watateuliwa kushiriki Mafunzo hayo huko Ihemi.
UVCCM
tunarejea kusema tena kwamba dhamira ya maandamano yetu ya kusifu Utendaji wa
Serikali ya awamu ya tano iko pale pale ila tutapanga tarehe nyingine katika
wakati ujao badala ya kufanyika Agosti 31 mwaka huu kama tulivyotangaza
hapo awali.
UVCCM
tunawataka Vijana wote kuendelea kuheshimu Tunu ya Amani Umoja na Mshikamo wetu
kwa Taifa.
KIDUMU
CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu
Shaka (MNEC)
KAIMU
KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment