Sunday, August 14, 2016

MZEE ABOUD JUMBE MWINYI, AFARIKI DUNIA.

Aliyekuwa Rais wa awamu ya pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza  la mapinduzi Zanziba, Aboud Jumbe  Mwinyi, amefariki dunia hii leo nyumbani kwake mji mwema,  wilaya  ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, Taarifa ya  kufariki kiongozi huyo ambae pia aliwahi kuwa makamo wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziliinea kwenye  mitandao ya kijamii mchana wa  leo.

Kufuatia Kifo hicho cha Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Dkt. John Pombe  Magufuli amemtumia salama za rambi rambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dkt. Aliy Mohamed Sheni.

Marehemu mzee Aboud Jumbe ambae alizaliwa Tarehe 14 juni 1920 amefariki akiwa na miaka 96 ambapo katika uhai wake alikuwa Rais wa pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na makamo wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, (7 Aprili 1972 hadi 30 Januari 1984).

Katika salamu zake za rambi rambi Rais Magufuli alimtaja marehemu Aboud Jumbe kuwa  ni mtu mwenye mchango kubwa kwa Taifa  la Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa ni miongoni mwa watu walioshiriki kupigania Uhuru wa Tanganyika.

Aidha, Rais Magufuli aliongeza kuwa  Marehemu Aboud Jumbe alikuwa ni mtu aliyejitoa kupigania  Uhuru, Haki, na maendeleo ya watu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Marehemu Mzee Aboud Jumbe  Mwinyi wakati uhai wake alitoa wasia ya kwamba pindi atakapofariki  katika mazishi yake kusiwe na bendi za muziki, wala kusipigwe mizinga na kuongeza kuwa jeneza lake lisifunikwe na bendera ya Taifa wala ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wasia huo wa marehemu Aboud Jumbe aliutoa  wakati wa mazishi ya aliyekuwa  rais wa awamu ya nne wa Zanzibar aliyefariki tarehe 15 Machi 2000.

Mungu ailaze roho ya Marehemu Aboud Jumbe  Mwinyi peponi, Aamiyn. Innaa lillaahi Wa innaa ilayhi Rajiuun. (Hakika sisi sote ni wa MwenyeziMungu na kwake yeye tutarejea).

No comments:

Post a Comment