Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb), akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu
Ukaguzi wa Maduka ya kubadilisha Fedha za Kigeni ambapo alisema lengo lake sio
kufuta biashara ya maduka hayo bali ni kudhibiti ukiukwaji washeria uliokithiri
na utakasishaji wa Fedha haramu.
...................................
Katika kutekeleza majukumu yake ya
kuhakikisha kuwa Sekta ya Fedha inachangia ipasavyo utulivu na ukuaji wa uchumi
nchini, Benki Kuu ya Tanzania ilibaini uwepo wa maduka ya kubadilisha fedha za
kigeni ambayo yalikuwa yakiendeshwa pasipo kuzingatia Sheria ya Foreign
Exchange Act 1992, Kanuni za The Foreign Exchange (Bureau de Change)
Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017 na Taratibu za utoaji wa
huduma za ubadilishaji wa fedha za kigeni.
Kufuatia hali hiyo, zoezi maalum la
ukaguzi wa kina kwa maduka hayo lilifanyika Arusha Novemba 2018 na kwa Dar es
Salaam siku ya tarehe 27 Februari 2019, 1 na 8 Machi 2019 kwa kuhusisha vyombo
vya Dola na kubaini ukwepaji mkubwa wa kodi na uvunjaji wa Sheria.
Zoezi hili limebaini pia uondoshwaji wa
fedha katika mfumo rasmi wa fedha na kuelekezwa kwenye mifumo ya utakasishaji
wa fedha haramu, kupokea Amana kutoka kwa wafanyabiashara kinyume cha matakwa
ya leseni za biashara husika, kudhoofisha thamani ya shilingi, pamoja na mambo
mengine ambayo yalianza kuathiri usalama wa nchi kwa ujumla.
Kwa mfano, baadhi
ya maduka yaligundulika kutumia fedha nyingi za Tanzania kununua fedha za
kigeni lakini fedha kidogo za kigeni ziliuzwa na hakuna taarifa ya matumizi ya
fedha za kigeni zilizobaki.
Ni vizuri ieleweke kuwa, zoezi
la ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni lilitekelezwa kwa
kuzingatia Sheria za nchi tofauti na malalamiko na tuhuma mbalimbali
zilizotolewa za kudai uwepo wa ukiukwaji wa Sheria na haki kwa wamiliki wa
maduka hayo.
Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna mmiliki yeyote wa duka
aliyewasilisha malalamiko kuhusiana na zoezi hili kwenye mamlaka husika. Hata
hivyo, Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka nyingine za Serikali zinafuatilia kwa
umakini ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo zinazotolewa.
Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza
majukumu yake kwa umakini. Hivyo, Serikali inauthibitishia umma wa Watanzania
kuwa katika zoezi la ukaguzi wa Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni hakuna
fedha au mali yeyote iliyotaifishwa.
Taratibu za kisheria zilifuatwa wakati wa
kuchukua vielelezo mbalimbali zikiwemo fedha, kompyuta, simu za viganjani,
mashine maalum za kuhifadhi taarifa na taarifa mbalimbali ili kusaidia
uchunguzi.
Aidha, lengo la zoezi hili sio kufuta biashara ya maduka ya
kubadilishia fedha za kigeni kwa watu binafsi, bali ni kudhibiti ukiukwaji wa
sheria uliokithiri, ukwepaji wa kodi na utakatishaji wa fedha haramu.
Maduka
machache ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo yalizingatia Sheria na Kanuni za
Foreign Exchange na masharti ya biashara hiyo yaliachwa kuendelea na
utoaji wa huduma hiyo.
Hivi sasa Serikali imeandaa Kanuni
mpya kwa ajili ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo
zitaelekeza jinsi ya kuomba leseni za uendeshaji wa maduka hayo kwa mtu binafsi
au taasisi yeyote na masharti ya kuzingatiwa wakati wa shughuli hizo.
Kanuni hizo zinalenga kuweka
mazingira mazuri ya biashara ambayo hayatatoa athari kwa sekta ya fedha na
uchumi jumla, na inakuwa yenye manufaa kwa nchi.
Kwa kuzingatia maduka mengi
yaliyokaguliwa yamefungwa, Benki Kuu ya Tanzania imechukua tahadhari ya
kuhakikisha huduma ya ubadilishaji fedha za kigeni inaendelea nchini kwa
kutolewa na benki zote pamoja na Shirika la Posta.
Benki Kuu ya Tanzania
itakuwa inatoa taarifa kuhusu upatikanaji wa huduma hiyo na kuzihimiza benki za
biashara na Shirika la Posta kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na huduma katika
maduka yaliyofunguliwa na benki hizo na Ofisi ya Posta.
Kwa kipindi kifupi cha utekelezaji wa
zoezi la udhibiti wa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni, thamani ya
shilingi imeimarika na upatikanaji wa fedha za kigeni katika benki za biashara
umekuwa mzuri.
Kabla ya zoezi la udhibiti wa biashara ya kubadilisha fedha ya
kigeni dola ya Marekani ilikuwa inauzwa kwa wastani wa shilingi 2,450 na baada
ya utekelezaji wa zoezi hivi sasa dola ya Marekani inauzwa kwa wastani wa
shilingi 2,300.
Aidha, Benki za biashara kwa wastani hivi sasa zinakusanya
jumla ya dola za Marekani milioni 15 kwa siku. Ni matarajio ya Serikali kuwa
udhibiti huu utaziwezesha Benki za biashara na taasisi nyingine kuuza fedha za
kigeni kwa wingi kwenye soko la fedha za kigeni na hatimaye kuongeza akiba ya
fedha za kigeni.
Serikali inatoa tahadhari kwa
wananchi kutoshiriki kwenye biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa njia
zisizo halali. Hivi sasa kuna taarifa kwa baadhi ya maeneo ya mipakani na
majiji ya Dar es Salaam na Arusha wamejitokeza watu wanaofanya biashara haramu
ya kubadilisha fedha za kigeni ambao wamewaathiri baadhi ya wananchi kwa wizi.
Vyombo vya usalama ikiwemo jeshi la polisi vimeongeza nguvu katika kuhakikisha
biashara hii haramu (Black Market) inatokomezwa na hivi sasa wahalifu saba
wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.
Serikali inapenda kuwahakikishia
Watanzania wote kuwa inayo akiba ya fedha za kigeni ya kutosha zipatazo dola za
Marekani bilioni 4.67 hadi tarehe 30 Machi 2019 zenye uwezo wa kuagiza bidhaa
na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisicho pungua miezi 4.8.
Hivyo,
wasiwasi kuwa Serikali imechukua hatua ya kufunga baadhi ya maduka ya
kubadilisha fedha za kigeni kwa sababu haina akiba ya fedha za kigeni si ya
kweli hata kidogo.
Aidha, hofu kwamba nchi inarejea katika kipindi cha nyuma
ambapo fedha za kigeni zilikuwa zinatolewa kwa vibali (rationing) ili kukidhi
mahitaji ya fedha hizo kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, nazo
hazina msingi.
Mapato ya Nchi yanayotokana na vyanzo
vya fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi yalikuwa na thamani
ya dola za Marekani milioni 8,554.5 kwa mwaka unaishia Februari 2019 ikiwa ni
ongezeko la asilimia 1.4 ikilinganishwa na fedha za kigeni zilizopatika mwaka
unaishia Februari 2018.
Ongezeko hilo la mapato ya fedha za kigeni kwa Nchi
yamechangiwa zaidi na uuzaji wa bidhaa zisizo asilia nje ya nchi zikiwa na
thamani ya dola za Marekani milioni 3,878.5 sawa na asilimia 10.3
ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Vile vile, huduma zilizotolewa nje ya
nchi kama vile usafiri na usafirishaji na utalii ziliingiza jumla ya dola za
Marekani milioni 4,074.1 sawa na ongezeko la asilimia 6.1 ikilinganishwa kiasi
kilichopatikana mwaka ulitangulia.
Aidha, Serikali inachukua fursa hii
kuwaeleza wananchi kuwa nchi yetu ina akiba ya chakula cha kutosha ambacho kina
utoshelevu wa asilimia 124 kwa mwaka huu wa fedha 2018/19. Hivyo,
Serikali haitarajii kutumia fedha za kigeni kuagiza chakula kutoka nje ya nchi
isipokuwa tu kama ikitokea hali ya ukame ikawa mbaya katika siku zijazo.
Serikali, kupitia Benki Kuu ya
Tanzania, inawataka wafanyabiashara ya huduma ya kubadilisha fedha za kigeni
kuzingatia na kutii Sheria ya Foreign Exchange 1992, Kanuni ya Foreign
Exchange (Bureau de Change) Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017,
Masharti ya biashara ya huduma ya kubadilisha fedha za kigeni na Maelekezo ya
Msimamizi (BOT) wa Sekta ya Fedha Nchi.
Mwisho Serikali inawapongeza wananchi
wa Tanzania kwa kuwa waelewa na watulivu wakati wote zoezi la ukaguzi
likiendelea, licha ya kujitokeza kwa taarifa za upotoshwaji wa zoezi hili.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof.
Florens Luoga, akieleza kuwa jumla ya maduka 87 yamefanyiwa ukaguzi Jijini Dar
es Salaam na ni maduka matano pekee ndio yamebainika kutokiuka sheria, wakati
wa mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango
(Mb), na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini
Dodoma.
Baadhi ya Waandishi wa Habari na Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Benny
Mwaipaja (kushoto), wakiwa katika Mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ambapo Waziri huyo alisema hakuna mmliki wa Duka
la Kubadilisha Fedha ambaye amewasilisha malalamiko yoyote kwa mamlaka husika
kuhusu zoezi la ukaguzi wa maduka hayo.
No comments:
Post a Comment