Binti mwenye umri wa miaka 25, Mariam
Rajab mkazi wa kitongji cha Inung'una mkoani Singida, aliyeteseka kwa muda
mrefu na kidonda mgongoni, ambaye video yake ilisambaa kwenye mitandao ya
kijamii akiomba msaada wa matibabu, hatimaye amepokelewa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH), saa sita usiku wa jana, Jumatano.
Mariam amepokelewa katika Idara ya
Magonjwa ya Dharura, ambapo kwa sasa anaendelea kufanyiwa vipimo vya awali na kisha atalazwa, ili aweze kuonana na jopo la madaktari
bingwa wa upasuaji kwa ajili ya kupatiwa matatibu zaidi.
Msemaji wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Aminiel Algaesha amesema matibabu ya mgonjwa huyo
yatagharimiwa na hospitali hiyo.
Kupitia video yake iliyosambaa katika
mitandao ya kijamii, binti huyo alijieleza namna anavyoteseka na kidonda hicho.
“Mimi naitwa Mariam Rajabu naishi
katika Mkoa wa Singida, Mtaa wa Mnung’una naishi katika familia ya kimasikini,
wazazi wangu hawana uwezo wa kunisaidia tatizo langu, tatizo ambalo ninalo,
tatizo lenyewe ambalo ninalo ni kidonda ambacho kipo hapa mgongoni, naombeni
Watanzania wenzangu muweze kunisaidia niweze kwenda hospitali ya Muhimbili ili
niweze kupata matibabu.Sina cha kuwalipa bali Mungu atawalipa, asanteni”
Baada ya kuonekana kwa video hiyo,
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
aliuagiza uongozi wa MNH kumtafuta Mariam popote alipo ili apelekwe hospitalini
hapo kwa ajili uchunguzi na matibabu.
Mariam ameletwa Muhimbili kwa gari la
wagonjwa kutoka mkoani Singida, lililoanza safari yake saa 8:00 mchana jana.
Mariam
Rajab (25) akipokelewa na wahudumu wa Afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
No comments:
Post a Comment