Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof Joyce Ndalichako(Katikati) akikata utepe
kuashiria uzinduzi wa Jengo Jipya la Kufundishia lililojengwa na chuo hicho kwa
gharama za mapato ya Ndani kulia kwake ni
Mwenyekiti
wa Bodi ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephene Wasira
..................................
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako amezindua ukumbi wa mihadhara wa kisasa katika Chuo Cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere uliojengwa mapato ya ndani ya Chuo hicho.
Akizundua ukumbi huo wa Mihadhara
kigamboni jijini Dar es salaam Waziri Ndalichako amepongeza Bodi ya Utawala na
Uongozi wa Chuo hicho kwa kusimamia vema matumizi ya fedha zinazotokana na
Mapato ya ndani na kutumia kutekeleza miradi yenye
tija kwa Chuo na Taifa kama ilivyofanyika katika ujenzi wa Ukumbi huo na pia
amewataka uongozi kusimamia Dira na Dhima ya uanzishwaji wake kwa kujikita
katika kutoa mafunzo ya Uongozi, Utawala na Maadili.
Waziri Ndalichako amewapongeza
Watendaji wa Chuo kwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Mradi huo hadi
kufikia hatua ya kukamilisha japo kwa kuchelewa kwa karibu miezi tisa.
“ nimefurahishwa na kazi hii nzuri
iliyofanyika hapa, kwakweli ni jengo zuri lenye ubora wa hali ya juu na ambalo
litawafanya wanafunzi kuongeza ari ya kujifunza na ninategemea kuona jengo hili
likituzwa vizuri ili litumike kwa miaka mingi likiwa na ubora uleule”.
Amesisitiza Ndalichako
Aidha Ndalichako amezitaka Taasisi
zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuthamini na kutumia
vizuri mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutekeleza mipango na Miradi
mbalimbali ya Maendeleo katika taasisi hizo ili kuleta maendeleo ya haraka
badala ya kuzitumia fedha hizo kwa matumizi mengine yasiyo na tija.
Wakati huo amewataka Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA) ambao ni wakandarasi wa ujenzi wa Ukumbi huo kukamilisha
miradi mingine iliyo chini ya Wizara ya Elimu ikiwemo ukarabati wa shule Kongwe
mfano Kibaha Sekondari, Shule ya Sekondari ya Wasichana Songea pamoja na ujenzi
wa Hosteli na miundombinu mingine katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Mloganzila.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Utawala ya
Chuo hicho Stephen Wasira, amesema Chuo hicho kimejipanga kuhahakisha kinatoa
elimu bora na wahitimu walio bora wenye weledi hasa katika eneo la uongozi na
utawala ili kuenzi fikra na maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere alieanzisha chuo hicho Mwaka 1961 kwa lengo la kuandaa viongozi na
watawala.
Awali, Mkuu wa Chuo Prof. Shadrack
Mwakalila akitoa taarifa ya mradi amesema jengo hilo limegharimu zaidi ya
Shilingi za Tanzania Bilioni 1.1 na kwamba lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 330
kwa wakati mmoja. Ameongeza kuwa pamoja na ukumbi wa Mihadhara jengo hilo lina
ofisi nane za wahadhiri na mifumo ya kisasa ya sauti.
No comments:
Post a Comment