Tuesday, April 30, 2019

WEKA HATA MTI UWEKEWE UMEME- DKT. KALEMANI

Na Omary Mngindo, Miono

WAZIRI wa Nishati DKT. Medard Kalemani amewataka wakazi katika vijiji vilivyopo Kata ya Miono Jimbo la Chalinze Mkoa wa Pwani, ambao havijapatiwa huduma huku wakiwa na maeneo ambayo hawajajenga, kuweke hata mti, ili washushiwe huduma hiyo.

Waziri Dkt. Kalemani ametoa kauli hiyo juzi alipofanya ziara ya siku moja ya kuwasha umeme katika nyumba mbili za wakazi katika Kijiji cha Makao Makuu katani humo, akiambatana na mwenyeji wake Ridhiwani Kikwete mbunge wa jimbo la Chalinze mkoani hapa.

Aidha Waziri huyo ametoa mwezi mmoja kwa Meneja wa shirikanla umeme nchini Tanesco (tawi la Chalinze) na Mkandarasi kuhakikisha wanamalizia kusambaza huduma hiyo katika vijiji vyote vilivyosalia, huku akiahidi kurejea hapo mwezi ujao kufuatilia agizo lake.

"Sijaridhishwa na kazi inayofanywa ndani ya Kata hii ya Miono, haiwezekani mradi huu ndani ya miezi 11viunganishwe vijiji viwili tu, serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 29, kazi yenyewe haieleweki, kuanzia kesho wekeni kambi hapa Miono, kazi ifanywe na vijana wa hapa," alisema Waziri huyo.

Pia Waziri Kalemani amewaambia wananchi hao kuwa, kuanzia sasa uunganishwaji wa umeme ni sh. 27,000 tu, uwe wa Tanesco au Rea huku akiahidi kupiga mnada wa kuku wa mkazi ambaye atashindwa kulipia kiasi hicho kwa ajili ya kuunganishiwa huduma hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani hakusita kumpongeza Waziri kwa namna wanavyosambaza huduma hiyo, huku akisema kuwa anaridhishwa na juhudi hizo na kuongeza kuwa kwenye maeneo kadhaa jimboni humo bado kuna uhitaji mkubwa wa upatikanaji wa umeme.

"Hapa kuna baadhi ya maeneo bado hayajafikiwa na huduma hii, leo asubuhi nimezungumza na wasaidizi wako wamenieleza kwamba kuna mradi wa ujazilizi, imani yangu ni kwamba mpango huo utayapitia maeneo hayo, pia kuna vijiji vingi ndani ya jimbo zima la Chalinze," alisema Ridhiwani.

Diwani wa Kata hiyo Juma Mpwimbwi amemuomba Waziri Kalemani kuwaongezwa nguzo japo 40 zitazopelekwa katika vitongoji vya Mwanakibungo na mifugoni ambavyo havijapitiwa kabisa na huduma hiyo.

Mmoja wa wakazi kijijini hapo Salumu Helman akizungumza baada ya mkutano huo alielezea furaha yake ya kupunguzwa kwa gharama ya uunganishwaji wa huduma hiyo pasipokujali unatokea Rea au Tanesco.
 Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwaniakizungumza mbele ya waziri wa Nishati kata ya Miono.

No comments:

Post a Comment