Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Hassan Suluhu akihutubia wananchi wa Songwe walioshiriki
kwa wingi katika uwanja wa Kimondo – Forest, Wilayani Mbozi kushuhudia uzinduzi
wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2019.
...............................
Na; OWM (KVAU) – SONGWE
Serikali imedhamiria kuimarisha
upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio mijini kufikia asilimia
95 na vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Hassan Suluhu wakati
wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Aprili 2, 2019 zilizofanyika uwanja wa
Kimondo – Forest Mlowo, Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru
mwaka huu 2019 isemayo “Maji ni Haki ya kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na
Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”
Makamu wa Rais amesema kuwa dhamira
ya Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kuboresha
huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu, afya, barabara, umeme vijijini,
usafiri wa anga, uvuvi, kilimo, viwanda na upatikanaji wa huduma ya maji safi
na salama kwa wote.
“Sera yetu ya Maji ya mwaka 2002
inasisitiza upatikanaji wa maji safi na salama ambayo ni muhimu kwa maisha ya
kila mtu, shughuli za kiuchumi na ustawi wa mazingira,” alisema Makamu wa Rais.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa
maji safi, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi
mbalimbali ya maji nchini ikiwemo mabwawa ya kimkakati na kuboresha miundombinu
ya uzalishaji na usambazaji maji safi.
Aidha, Makamu wa Rais alitoa wito kwa
Wananchi kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji kwa kuacha kufanya shughuli za
kibinadamu kando ya vyanzo hivyo.
Kupitia hadhara ya Uzinduzi wa Mbio
za Mwenge wa Uhuru Makamu wa Rais, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na
kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao ni muhimu katika kuleta
maendeleo ya watu na huduma za kijamii.
Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ndio msingi mkubwa wa amani, Mshikamano, Uzalendo
na Umoja tulionao katika Taifa.
“Tunu hii imekuwa ni kichocheo cha
maendeleo kwa wananchi na wamekuwa wakihamasika kushiriki katika kuandaa na
kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ya kijamii na kiuchumi
iliyopo katika maeneo yao,” alisema Mhagama.
Waziri Mhagama aliongeza kwa
kuwashukuru wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha tukio hilo muhimu la
Kitaifa.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Songwe, Brigedia Jenerali (Mst.), Nicodemus Mwangela alishukuru Serikali kwa kuchagua
Mkoa wa Songwe kuwa wenyeji wa Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa
mwaka 2019.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa Mkoa wa Songwe waliohudhuria
katika hafla ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista
Mhagama akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Songwe walioshiriki kwenye hafla ya
Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2019.
Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Balozi Ali Karume akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye Uwanja wa Kimondo, Wilayani Mbozi Aprili 2, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali
(Mst.), Nicodemus Mwangela akieleza jambo kuhusu Mkoa wa Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali
(Mst.), Nicodemus Mwangela akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa Mbio
za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bw. Mzee Mkongea Ali baada ya kukabidhiwa na Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Hassan Suluhu wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge zilizofanyika Aprili 2, 2019 Mkoani Songwe
katika Uwanja wa Kimondo.
Sehemu ya Vijana wenye dhamana ya kukimbiza
Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019 (waliosimama mstari wa mbele).
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment