Serikali kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali imeendelea na mkakati wake wa kuwajengea uwezo wananchi
illi waweze kupata taaluma na kuweza kushiriki kwenye sekta ya mafuta na gesi.
Akizungumza Bungeni jijini
Dodoma, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgallu alisema kuwa
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuvitumia vyuo
vilivyopo nchini kuwajengea uwezo wa kitaaluma wananchi katika masuala ya
utafutaji, uendelezaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji
wa mafuta na gesi asilia.
Naibu Waziri Mgallu alisema,
“Kwa mfano mwaka 2010 Kampuni ya Petrobras ilitumia dola za kimarekani 350,000
sawa na shilingi milioni 780 kufundisha na kukipatia Chuo cha VETA Mtwara vifaa
vya mafunzo.
Aidha, kupitia mpango huo, wanafunzi 50 na wakufunzi 2
walifundishwa kwenye fani ya umeme na makanika”.
Aidha, Kampuni ya Statoil imekuwa
ikifadhili mafunzo mbalimbali kwa ngazi ya vyuo, ambapo mwaka 2013 ilifadhili
wananchi 9 kusoma Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika
masuala ya fedha na uchumi wa mafuta ya gesi asilia.
Sambamba na hilo, mwaka 2012
Kampuni ya BG iliendesha mafunzo mbalimbali katika Chuo cha VETA mkoani
Mtwara, ikiwa ni pamoja na ufadhili wa mwaka 2012/2013 uliotolewa na iliyokuwa
Wizara ya Nishati na Madini kwa wanafunzi 50 katika chuo hicho.
Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) imefungua klabu 32 za
mafuta na gesi katika shule za Sekondari za mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo
la kutoa elimu inayohusu tasnia ya mafuta na gesi asilia pamoja na namna
inavyoweza kuwanufaisha kupitia fursa zinazotengenezwa na tasnia hiyo katika
maeneo yao.
No comments:
Post a Comment