Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi William Lukuvi amesema kuanzia sasa gharama za urasimishaji haitazidi
shilingi 150,000 badala ya 250,000 iliyopangwa awali na makampuni yatakayoenda
kinyume yatachukuliwa hatua ikiwemo kufutwa.
Lukuvi alitoa kauli hiyo jana Aprili 17, 2019. jijini
Dar es Salaam alipokutana na Makampuni ya Upangaji na Upimaji yanayofanya kazi
ya urasimishaji katika mitaa mbalimbali nchini pamoja na watendaji wa sekta ya
ardhi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, baada ya Wizara
yake kuona zoezi la urasimishaji linasuasua wamegundua asilimia 30 pekee ndiyo
iliyorasimishwa tangu kuanza zoezi hilo na hali hiyo imechangiwa na uwezo mdogo
wa wananchi wengi kumudu gharama za urasimishaji.
Waziri Lukuvi alisema, alichotegemea
kwa makampuni yaliyopewa kazi ya urasimishaji ni kuwa na uzalendo kwa kushusha
gharama lakini yameshindwa kupunguza gharama jambo lililoifanya serikali kuona
haja ya kupitia upya gharama hizo na kubaini gharama za msingi ili kumuwezesha
mwananchi kupata hati na kusisitiza punguzo hilo halitawahusu waliolipia
gharama za urasimishaji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi ameyataka makampuni yanaoyoendesha zoezi la urasimishaji kuhakikisha
kiasi cha fedha inachowatoza wananchi kinaishia hatua ya Hati na gharama
itakayolipwa na mwananchi baada ya kurasimishwa ni kodi ya ardhi na
kuyatahadharisha kutochukua muda mrefu kukamilisha zoezi hilo.
Amewataka wananchi wote wanaoishi
kwenye maeneo yasiyo rasmi kuhakikisha wanaingia katika zoezi la urasimishaji
ili kupata hati itakayowawezesha kiuchumi na kusisitiza kuwa suala hilo
linafanyika kwa nia njema kwa nia ya kuwaongezea mtaji wananchi kwa kupatiwa
nyaraka itakayowasiadia kukopa fedha benki.
No comments:
Post a Comment