NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA
MKUU wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama, amewaasa madereva wa pikipiki
maarufu kama bodaboda, kulipia vitambulisho vya wajasiriamali na endapo
watashindwa kufanya hivyo hawataruhusiwa kufanya biashara ya kubeba abiria.
Mkuu huyo wa wilaya aliyasema hayo mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na madereva hao na
kusema, wao ni moja ya kundi ambalo linapaswa kuwa na vitambulisho vya
wafanyabiashara wadogo ambapo wanatakiwa kulipia shilingi 20,000.
Mshama alisema kuwa agizo la watu wanaofanya biashara ambayo mtaji wake
hauzidi kiasi cha sh.milioni nne wanapaswa kuwa na vitambulisho hivyo.
“Mnapaswa kununua vitambulisho hivyo na kwa wale ambao hawatakuwa na
vitambulisho hivyo hawataruhusiwa kufanya biashara hiyo hivyo hakuna budi kila
mmoja wetu kuhakikisha analipia kiasi hicho ili waweze kufanya kazi bila ya
usumbufu,” alisema Mshama.
Aliwataka wafanyabiashara wengine nao kulipa ili wapatiwe vitambulisho
ambavyo Rais ametaka wajasiriamali wadogo wawe navyo kwani nao wanachangia
uchumi wa taifa.
“Tunaendelea kuwahamasisha wajasiriamali wadogo wachangamkie fursa hiyo
kwani ushuru waliokuwa wakilipa kwa sasa utakuwa haupo na kitambulisho hicho
ndicho kitakuwa kimefidia na haitaruhusiwa kufanya bishara kama hawana
vitambulisho hivyo,” alisema Mshama.
Kwa upande wake Bakari Kapera wa kitengo cha elimu ya mlipa kodi kutoka
mamlaka ya mapato (TRA) mkoa wa Pwani alisema kuwa fedha wanazolipia
leseni siyo kodi bali ni ada ili mtu kutambulika kuwa ni dereva.
Kapera alisema Leseni ya udereva ni tofauti na kitambulisho cha Ujasiriamli hivyo aliwataka madereva hao wasikwepe kutekeleza agizo hilo kwa kisingizio kuwa tayari wamelipia leseni za udereva.
Stanley
Ndunguru kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga na Majini (SUMATRA)
alisema kuwa malipo hayo yanalipwa na mmiliki wa chombo na siyo wao kama
madereva kwani hawaruhusiwi kulipa ikiwa ni pamoja na bima.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Jenifa Omolo alisema
kuwa waendesha boda boda nao wametajwa kuwa nao ni mwiongoni mwa wanaotakiwa
kulipia vitambulisho hivyo.
Katibu wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Pikipiki
wilaya ya Kibaha (CHAWAMAPIKI) Shaban Kambi alisema kuwa kilichosababisha
wakashindwa kuchukua vitambulisho hivyo ni kutopatiwa elimu juu ya wanaopaswa
kulipia.
No comments:
Post a Comment