Thursday, April 25, 2019

WAANDISHI WATAKIWA KUFUATA MAADILI NA SHERIA ZA UANDISHI KATIKA VYOMBO VYA HABARI

Baraza la Habari Tanzania (MCT)  limewataka waandishi pamoja na wahariri hapa nchini waweze kuwa makini katika uandaaji wa taarifa ambazo zinakidhi kiwango na zenye maadili ya uandishi na pia zisiegemee upande mmoja kwani kunaweza kumsababishia kuingia kwenye wakati mgumu.


Hayo yamesemwa leo katika uzinduzi wa machapisho ya vitabu ambavyo vimetoa ripoti mbalimbali juu ya uhuru wa wanahabari katika vyombo vya habari hapa nchini hasa kutokana na matukio mbalimbali yaliyojitokeza hivi karibu ikiwemo kupotea kwa waandishi na wengine kutishiwa.


Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Jaji Mstaafu Juxon Mlay amesema kuwa tunalinda na kutetea uhuru wa wanahabari kwaajili ya wananchi kupata habari na si kwaajili ya wanahabari pekee.


“Mazingira ya sasa ni magumu katika tasnia ya uandishi wa habari, sasa yale ambayo yameandikwa kwa kutuonya, kutuelekeza na kutukumbusha humu ni muhimu kwetu ili tuweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya sasa wakati huohuo tukiwa tukijalibu kupambana na kushirikiana na wale wenye mamlaka ili kuboresha haya mazingira ya kufanya kazi zetu”. Amesema Bw.Mlay.


Kwa upande wa mwandishi wa chapisho la taarifa inayomhusu mwandishi wa Channel Ten Geofrey Nilahi ambaye alikuwa Ruvuma, Bw. Attilio Tagalile amesema kuwa mwaka jana mwandishi huyo aliwaandikia viongozi wa MCT ya kuwa maisha yake yapo hatarini kutokana na kazi ambayo anaifanya hasa kutokana na kutoa taarifa ambayo ilikuwa inamkwaruzano baina ya wananchi na serikali.


“Alikuwa ameandika taarifa za kichunguzi zilikuwa zinaonyesha matatizo yaliyokuwa katika maeneo yale ambapo matatizo hayo ni pamoja na matatizo ya shule kutokana na wanafunzi kusoma katika mazingira magumu ikiwa jimbo hilo lina viongozi wakubwa”. Amesema Tagalile.


“Yeye anavyodai ni kwamba baada ya kupata stori zake alijaribu kupata wahusika ili aweze kubalansi stori zake kwamaana ya wabunge pamoja na wakuu wa wilaya na vilevile. Mbuge wa jimbo la Peramiho Jenista Mhagama alitumiwa ujumbe mara mbili lakini hakujibiwa”. Ameongeza Tagalile.


Hata hivyo Bw. Tagalile amesema kuwa waandishi walishiriki kufuta ile taarifa ambayo ameiandika mwandishi Nilahi, waandishi ambao walikuwa wanatakiwa kumuunga mkono kwa harakati zake lakini chakushangaza wao ndo wanakuwa chanzo cha kumkandamiza mwenzao.


Kwa upande wa Bi. Pili Mtambalike amesema ripoti ambayo ameia imelandaa imelenga kuangalia changamoto mbalimbali ambazo vyombo vya habari vimepitia ikiwemo masuala ya sheria,masuala ya sera za nchi pamoja na changamoto mbalimbali zitokanazo na sheria za vyombo vya habari.


“Hivi karibuni gazeti la Citizen lilifungiwa baada ya kuandika masuala ya uchumi, masuala ya uchumi si rahisi kukosewakosewa kwasababu kuna wachumi waliobobea ambao unaweza kuwauliza pia kuna takwimu zinatolewa na benki kuu pamoja na wizara husika na kama ni mwandishi mzuri ukiziandika zile huwezi kuwa na mashaka na taarifa yako”. Ameongeza Bi. Pili.


Aidha kwa upande wa Bw. Absalom Kibanda amesema kuwa katika chapisho la ripoti ambalo ameliandaa limelenga kuwakumbusha wanahabari wajibu wao kitaaluma pamoja na kimaadili ambapo hali ya vyombo vya habari kwasasa kuna wasomi wengi kuliko zamani.


“Kwanini kuna kuwa na ukiukwaji wa kitaaluma pamoja na misingi ya kimaadili kuliko ilivyokuwa zamani ambapo wasomi walikuwa wachache na pengine hili kwasisi katika vyombo vya habari tunatakiwa tujitathimini kama tutatimiza wajibu wetu kitaaluma na vilevile kimaadili”. Amesema Kibanda.

No comments:

Post a Comment