Wednesday, April 10, 2019

RIPOTI ZA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA ULIOISHIA TAREHE 30 JUNI, 2018

MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad,akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma wakati akitoa Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha Ulioishia Tarehe 30,Juni,2018.
..................................


MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad,amesema kuwa katika ukaguzi uliofanyika kwa mwaka 2017/18 Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA  haikujumlisha shilingi bilioni 18.95 ambazo ni Vocha za Misamaha ya Kodi kutoka Hazina.


Prof.Assad ameyasema hayo leo Aprili 10, 2019. jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya za Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia juni 30 mwaka 2018.


Amesema  kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya shilingi trilioni 15.38 ikilinganishwa na malengo yaliyowekwa ya kukusanya shilingi trilioni 17.31; hivyo kuwa na nakisi ya makusanyo kwa shilingi trilioni 1.93 ambazo ni sawa na asilimia 11 ya malengo.


 Hivyo, makusanyo halisi ya mwaka 2017/18 ni shilingi trilioni 15.40 yakijumuisha na Vocha za Misamaha ya Kodi kutoka Hazina.


“Kodi zilizoshikiliwa katika Kesi za muda mrefu kwenye Mamlaka za Rufaa za Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania ina Mashauri ya Kodi ya Thamani ya shilingi trilioni 382.6 kwenye Mamlaka za Rufaa za Kodi ikiwa ni ongezeko la kiasi cha shilingi trilioni 378.2 (asilimia 8595) ikilinganishwa na shilingi trilioni 4.4 kwa mwaka wa fedha 2016/17”amesema Prof Assad.


Aidha amesema  kuwa ongezeko hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na mashauri manne yenye thamani ya shilingi trilioni 374.7 yanayoihusu Kampuni ya Uchimbaji Madini ya ACACIA.


“ Kutokukusanywa kwa mapato yatokanayo na kodi ya Kiasi cha Shilingi Bilioni 46.81 na Dola za Marekani Milioni 2.74, ukaguzi wangu ulibaini kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishindwa kukusanya mapato zaidi ya shilingi bilioni 46.81 kutoka kwa walipakodi mbalimbali.


 Kwa upande mwingine Prof.Assad amesema  kuwa wakati wa uhakiki wa bidhaa zinazoingizwa Nchini na Nchi jirani ili zisafirishwe kwenda Nchi nyingine, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishindwa kumpatia ushahidi kuthibitisha kuwa kodi ya shilingi bilioni 57.09 ililipwa.


“ Aidha, nilibaini kuwa bidhaa zilizosafirishwa kutoka nchini kwenda nchi nyingine zilizopaswa kutozwa kodi ya ongezeko la thamani ya shilingi milioni 649.45 ziliruhusiwa kwenda nje ya nchi bila kukamilisha taratibu za Forodha”amesisitiza


“Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishindwa kutoa ushahidi wa nyaraka za kuthibitisha kuwa kodi stahiki zilikusanywa. 3.2.2 Usimamizi wa Deni la Serikali Kufikia tarehe 30 Juni, 2018, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 50.92, ambapo deni la ndani lilikuwa shilingi trilioni 14.73 na deni la nje shilingi trilioni 36.19; kiasi hiki ni ongezeko la shilingi trilioni 4.84 sawa na asilimia 10.5 ikilinganishwa na deni la shilingi trilioni 46.08 lililoripotiwa tarehe 30 Juni, 2017”ameongeza Prof.Assad


Hata hivyo amesema  kuwa “Katika ukaguzi wangu, nilibaini masuala ya msingi yafuatayo kuhusu Deni la Serikali na usimamizi wake:


(a) Mapungufu katika usahihi wa taarifa kutokana na udhibiti wa ndani usiojitosheleza katika kuweka kumbukumbu na kutoa taarifa za Deni la Serikali.


(b) Serikali kuchelewa kulipa madeni ya Benki Kuu ya kiasi cha shilingi bilioni 212.7. Kati ya hizo, shilingi bilioni 199.79 zinatokana na riba ya nakisi ya Serikali, na shilingi bilioni 12.9 ikiwa ni sehemu ya Serikali ya gharama za kudhibiti ukwasi kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2017/18.


(c) Kutokuwapo kwa uwianishaji wa taarifa za mfumo wa malipo (Epicor) na Mfumo wa Utunzaji wa Taarifa za Deni la Taifa wa Jumuiya ya Madola (Common Wealth Secretariat-Debt Record Management System – (CS-DRMS)). Hii inasababisha taarifa za fedha kutowiana na vyanzo vyake, hivyo kuhatarisha uadilifu wa taarifa za Deni la Serikali.


Akiongelea  ukaguzi maalumu wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole (AFIS) alisema ulibaini mambo yafuatayo:


(a) Mahitaji ya kitaalamu kutoka idara inayotumia mfumo huo hayakuzingatiwa wakati wa kutathmini na kutoa zabuni.


(b) Malipo ya shilingi bilioni 3.30 yalifanyika kwa mzabuni kwa ajili ya huduma ya matengenezo na msaada wa kitaalamu wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole kwenye mikoa nane ya Kipolisi ya Temeke, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Kigoma, Geita, na Kinondoni lakini Jeshi la Polisi lilishindwa kuthibitisha kuwa matengenezo hayo na msaada wa kitaalamu ulifanyika. 45


(c) Vifaa vya Utambuzi wa Alama za Vidole vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.73 havikufungwa kwenye magereza 35 yaliyoainishwa. Badala yake vilihifadhiwa katika Ofisi ya Upelelezi, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.


(d) Malipo ya shilingi milioni 604.39 kwa ajili ya mafunzo kwa wataalamu 30 hayakufanyika.


(e) Jeshi la Polisi lilishindwa kuionesha timu yangu ya ukaguzi zilizo monita 58 za kompyuta aina ya Dell zenye thamani ya shilingi milioni 159.16 zilizopelekwa kwenye Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi (Forensic Unit). Pia, monita 213 za kompyuta aina ya Dell zililipiwa kiasi cha shilingi milioni 195.22 kwa mzabuni Lugumi Enterprises Limited lakini mzabuni hakuzileta.


Udhaifu katika Ukusanyaji wa Shilingi Bilioni 97.58 za Madeni ya
Alisema kuwa “Nilibaini kuwepo kwa kiwango kidogo cha kukusanya marejesho ya madeni ndani ya Mamlaka za Maji, kwa kuwa mapato mengi yalikuwa hayajakusanywa na yamezidi muda uliowekwa kwenye Sera ya Mikopo ya Mamlaka husika.


Katika jumla ya deni hilo la shilingi bilioni 97.58, nilibaini kuwa shilingi bilioni 39.59 (sawa na asilimia 41) ni Madeni ya Serikali, na shilingi bilioni 57.99 (sawa na asilimia 59) ni madeni ya wateja wengine.


Ongezeko hili la madeni limesababishwa na ufuatiliaji hafifu wa wadeni na kutokufuata Sera ya Mamlaka za Maji ya kukata huduma za maji kwa wateja wanaokiuka taratibu.


Hata hivyo amesema kuwa katika ukaguzi wangu, nilifanya tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya kiukaguzi yaliyotolewa miaka iliyopita na kubaini kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuyafanyia kazi.


Tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo hayo inaonesha kuwa kati ya mapendekezo 350 yaliyotolewa miaka iliyopita, mapendekezo 80 sawa na asilimia 22.9 yametekelezwa kikamilifu. Mapendekezo 124 sawa na asilimia 35.4, utekelezaji wake unaendelea.


 Prof.Assad amesema  kuwa, mapendekezo 72 sawa na asilimia 20.6 utekelezaji wake haujaanza; na mapendekezo 74 sawa na asilimia 21.1 yamepitwa na wakati.


Aidha amesema  kuwa katika Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyokuwa inatekelezwa na Taasisi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2017/18, “nimetoa jumla ya Hati za Ukaguzi 469. Kati ya hizi, Hati zinazoridhisha ni 455, sawa na asilimia 97; na Hati zenye shaka ni 14, sawa na asilimia 3” 

Zaidi Tembelea .http://www.nao.go.tz/?p=2081

 

No comments:

Post a Comment