Mariam Rajab Juma (25) akiwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) ambako ameanza kupatiwa matibabu ya kidonda kinachomsumbua
mgongoni sehemu ya bega la kulia. Wataalam wamesema atahamishwa Hospitali ya
Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu
zaidi.
Mariam akiwa wodini leo wakati waandishi wa
habari wakimhoji kuhusu maendeleo ya afya yake.
............................
Baada ya Mariam Rajab Juma (25), mkazi wa
Singinda kufanyiwa vipimo mbalimbali ili kubaini ugonjwa unaomsumbua, wataalam
wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wameshauri ahamishiwe Hospitali ya
Saratani ya Ocean Road kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Wiki iliyopita Mariam alifikishwa Muhimbili
akitokea mkoani Singida na kufanyiwa vipimo mbalimbali ili kubaini ugonjwa
unaomsumbua katika kidonda kilichopo sehemu ya bega la mkono wake wa kulia.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Daktari
Bingwa wa Upasuaji wa Muhimbili, Dkt. Ibrahim Mkoma amesema Mariam ataanza
matibabu rasmi katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na kwamba baada ya
kumaliza matibabu atarejeshwa Muhimbili kuendelea matibabu zaidi.
Dkt. Mkoma amefafanua Mariam atahamishiwa
Hospitali ya Saratani ya Ocean kwa kuwa kuna baadhi huduma za matibabu ambazo
anapaswa kupatiwa katika hospitali hiyo kutokana na ugonjwa unaomsumbua.
Daktari alipoulizwa kuhusu ugonjwa unaomsumbua
Mariam, Dkt. Mkoma amesema suala la ugonjwa ni siri ya mgonjwa na wataalam wa
hospitali na kwamba taratibu za hazimruhusu kuweka wazi aina ya ugonjwa
unaomsumbua mgonjwa.
Naye Mariam amesema amefurahishwa na huduma nzuri
ya matibabu aliyopatiwa na walaam wa Muhimbili kwani tangu alipofikishwa hapa
amekuwa akihudumiwa vizuri.
“Hivi sasa naendelea vizuri, tangu nimekuja
Muhimbili naendelea vizuri. Kabla sijafika Muhimbili nilikuwa siwezi kutembea
vizuri lakini sasa naweza kutembea vizuri,” amesema Mariam.
Mariam alifanyiwa vipimo vya CT-scan ya kifua na
kichwa, Ultrasound pamoja na vipimo mbalimbali vya damu ambavyo vimesaidia
kubaini ugonjwa unaomsumbua Mariam.
Dkt. Mkoma amesema kidonda kilichopo sehemu ya
mgongo wa Mariam ni kidonda sugu ambacho kilihitaji kufanyiwa vipimo mbalimbali
kubaini ugonjwa unaomsumbua.
Awali, Mariam amesema aliwahi kuugua moto akiwa
na umri wa miaka mitano ambapo alitibiwa na kupona ingawa alibaki na kovu kubwa
kuanzia sehemu ya mgongo wake hadi kwenye kisogo.
Amesema mwezi wa nane mwaka jana alipata kipele
kwenye kovu na baadae kipele hicho kugeuka kuwa jipu. Alipotumbua jipu lilitoa
usaha na kisha kuanza kuota kidonda kilichoendelea kuongezeka siku hadi siku.
“Nilienda kutibiwa katika Hospitali ya
Makiungu iliyopo Manispaa ya Singida, lakini pia kutokana na wazazi wangu
kutokua na uwezo wa kifedha niliacha kwenda hospitalini na kuanza kusafisha
kidonda mwenyewe, huku nikiwaomba marafiki zangu niliosoma nao sekondari
wanichangie fedha ili niweze kununua dawa,” amesema Mariam.
No comments:
Post a Comment