RAIS Dkt.
John Pombe Magufuli amesema Serikali haina mpango wa kuongeza maeneo ya utawala
ikiwemo kuanzisha mikoa mipya na badala yake imejipanga kuimarisha huduma na
mahitaji ya miundombinu iliyopo ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Namtumbo-Kilimasera-Matemanga-Tunduru
yenye urefu wa kilometa 193 leo (Ijumaa April 05, 2019), Rais Magufuli alisema
Serikali imekusudia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo
ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, maji, elimu n.k katika maeneo waliopo.
Aliongeza
kuwa katika awamu yake yake ya Uongozi, suala la kuongeza maeneo ya utawala
halipo na badala yake kuwataka Viongozi wa maeneo hayo wajipange katika
kuwaletea maendeleo wananchi badala ya fedha zilizopo kwenda katika kujenga
ofisi mpya za Wakuu wa Mikoa mipya na kuwalipa mishahara viongozi hao.
“Tumepanga
kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu, tumechelewa kuleta Maendeleo
hususani kwa wananchi wetu wa mikoa ya kusini, Serikali ninayoiongoza haina
mpango wa kuanzisha mikoa mipya , badala yake pesa hizo tutazielekeza katika
ununuzi wa madawa na kuboresha miundombinu ya barabara, elimu na nishati’
alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais
Magufuli alisema bado yapo baadhi ya maeneo mengi nchini yanakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo barabara za lami, hivyo Serikali haitoweza kuleta
Maendeleo katika sehemu moja kwa kuwa fedha hizo hazipo na kwamba ina
mahitaji makubwa katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi
katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa mujibu wa
Rais Magufuli alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa huduma muhimu na
za msingi kwa Maendeleo ya wananchi zinapewa kipaumbele ikiwemo ujenzi wa vituo
vya afya na Zahanati, kwa kuwa kukamilika kwake kutasaidia kupunguza vifo vya
akina mama na watoto ambavyo katika miaka ya nyuma vimekuwa vikisababisha vifo
vya makundi hayo ya kijamii.
Akizumgumzia
kuhusu Sekta ya Maji, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Maji, Prof. Makame
Mbarawa kuwasimamia wakandarasi wa miradi ya maji nchini, kwani Serikali
imekuwa ikitenga kiasi kikubwa cha cha fedha katika miradi ya Maendeleo pasipo
na kupata matokeo yaliyotarajiwa, na hivyo kuisababishia hasara Serikali.
“Kwa mujibu
wa ripoti ya Wizara ya Fedha na Mipango, miradi mingi ya maji imekuwa ikitumia
fedha nyingi pasipo na kupata matokeo yoyote na wataalamu wetu hasa wakandarasi
wamekuwa wazito kutoa tafsiri za nadharia za utaalamu na kuzileta katika
nadharia halisi, na mataifa ya nje yanashangwa tunaposhindwa kuvitumia vyanzo
tulivyonazo ili kuweza kuzalisha maji ya kutosha’ alisema Rais Magufuli.
Awali
akizungumzia kuhusu ujenzi wa barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema kujengwa kwa barabara hiyo kutaimarisha
mawasiliano katika ukanda wa kusini unaojumuisha Mtwara, Mingoyo, Masasi,
Mangaka, Tunduru hadi Mbamba Bay na hivyo kuzidi kufungua fursa za kiuchumi
nanchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Alisema hadi
kukamilika kwake barabara hiyo imegharimu kiasi cha Tsh Bilioni 173, ambapo
Shirika la Misaada la Japan limetoa asilima 23.24, Benki ya Maendeleo ya Afrika
asilimia63.32 na Serikali ya Tanzania asilimia 13.35 ikiwemo kodi na kulipa
fidia kwa wananchi wanaostahili kwa mujibu wa sheria ya barabara ya mwaka 2007.
Naye Balozi
wa Japan nchini Tanzania, Shinichi Goto alisema Serikali ya Japan imekuwa
mstari wa mbele kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo
barabara ya Namtumbo-Kilimasera-Matemanga-Tunduru na itaendelea kusaidia miradi
mingine ili kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuondoa
umaskini kwa wananchi wake yanafikiwa.
No comments:
Post a Comment