Watanzania wametakiwa kuwa na
utamaduni wa kupanda na kutunza miti, ili kujiondoa kwenye athari zinazotokana
na mabadiliko ya tabia nchi yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa
Rasilimali za Misitu na Nyuki Zawadi Mbwambo wakati wa maadhimisho ya siku ya
upandaji miti.
Mbwambo ambaye aliongoza wadau
mbalimbali kupanda miti katika eneo la Kilongawima Mbezi Beach jijini Dar es
Salaam amesema mabadiliko ya sasa ya hali ya hewa
ni matokeo ya uharibifu wa mazingira.
Amesema, “Hata mvua zinavyokuwa bila
mpangilio ni matokeo ya uharibifu huo, tumeona ipo haja ya kurekebisha hilo na
tunafanya kwa kupanda miti,”
“Mwaka huu tumeona tusifanye sherehe
za kitaifa kinachofanyika ni kuadhimishwa kikanda kila maeneo watu wanapanda
miti na hapa tulipo ni eneo la TFS linalosimamiwa na Kanda ya Mashariki,”
Amesema kwa mwaka huu TFS imeamua
kupanda miti katika maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na lengo la zoezi hilo ni
kuyarudishia kwenye uoto wake wa asili.
Katika eneo la Kilongawima ambalo ni
ukanda wa pwani jumla ya miti 1000 imepandwa ikiwemo mivinje na mikoko.
Kwa upande wake Meneja wa Misitu wa
Wilaya ya Kinondoni Dotto Ndumbikwa alitoa wito kwa jamii inayozunguka
kushirikiana na TFS kuitunza na kuilinda miti hiyo iliyopandwa, na kuahidi
kuimarisha doria ya pamoja, na kuwachukulia hatua wale wote watakaofanya
uharibifu wa miti kwa kuingiza mifugo kama vile ng'ombe na mbuzi.
No comments:
Post a Comment