KAMATI ya Marekebisho ya Katiba ya Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) imekamilisha hatua zote muhimu
kuhusu marekebisho ya katiba hiyo na sasa imeitisha mkutano wa wadau wote
Aprili 12 mwaka huu kwa ajili ya kuijadili na kuipitisha rasimu hiyo.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika ukumbi wa
Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Kamati ya Katiba ya TASWA inaamini mkutano
huo utakuwa na tija katika kuboresha rasimu hiyo ili taratibu zingine ziendelee
ikiwa ni pamoja na kupanga tarehe ya uchaguzi wa TASWA.
Kwa vile Kamati imekamilisha jukumu ililopewa la
kuandaa rasimu hiyo, hivyo kilichobaki ni ushirikiano kutoa kwa wadau ili
kumaliza jambo hilo.
Pamoja na mambo mengine rasimu hiyo
imeandaliwa kwa kuangalia Katiba za vyama mbalimbali duniani vinavyohusiana na
waandishi wa habari za michezo na pia kupitia muongozo kutoka Chama cha
Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS), ambacho TASWA ni
mwanachama.
Pia Kamati imechambua Katiba ya sasa
ya TASWA na kupokea maoni kutoka kwa waandishi wa habari za michezo kuhusu
maeneo yenye upungufu kwa nia ya kuiboresha.
Maeneo mbalimbali yamefanyiwa kazi katika
rasimu hiyo baadhi yakiwa ni sifa ya mwanachama, wajibu wa mwanachama, muundo
wa uongozi, sifa za viongozi na pia ukomo wa uongozi, pia kuna mapendekezo
katika rasimu hiyo ya kuanzishwa kamati mbalimbali kwa nia ya kuisaidia Kamati
ya Utendaji.
Kamati ya
Katiba ya TASWA imeundwa kutokana na agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyelitaka Baraza la Michezo Tanzania (BMT) lisitishe uchaguzi wa TASWA
uliokuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka jana na badala yake BMT ikutane
na viongozi wa TASWA pamoja na baadhi ya wanahabari wa michezo kuona namna ya
kuifanyia marekebisho Katiba ya TASWA iendane na wakati.
Kamati ya Katiba inayoongozwa na Mwenyeketi
wa zamani wa TASWA, Boniface Wambura ambaye pia ni Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), viongozi wengine ni Katibu wa Kamati Amir
Mhando ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TASWA na mwanahabari, Gift Macha ambaye ni
Katibu Msaidizi wa Kamati.
Wajumbe ni
Katibu Mkuu wa zamani wa TASWA, Abdul Mohammed, Mhazini wa zamani wa TASWA,
Nasongelya Kilyinga na wanahabari Thabit Zacharia na Devotha Kihwelu.
No comments:
Post a Comment