Kijana
mmoja mwenye umri wa miaka 21 Mkazi wa Mianzini B kata ya Kisutu wilayani
Bagamoyo (jina linahifadhiwa) amehukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kosa la
kushambulia mlango na kuvunja kioo cha mlango huo nyumbani kwa baba yake mzazi.
Upande
wa mashtaka ulidai mbele ya mahakama ya mwanzo Mwambao mjini Bagamoyo kuwa, mnamo
tarehe 19 mwezi Machi 2019 majira saa tano na nusu usiku huko nyumbani kwa baba wa mshitakiwa Kitongoji cha mianzini B kata ya Kisutu wilayani Bagamoyo mshtakiwa kwa
makusudi alitenda kosa hilo na kusababisha hasara ya shilingi 150,000.
Akitoa
maelezo ya kosa mbele ya mahakama, mlalamikaji ambae ni baba mzazi wa
mshitakiwa alisema mwanae huyo kutokana na matukio yake yasiyomridhisha
alilazimika kumuwekea utaratibu maalum wa makubaliano ili waweze kuishi kwa
pamoja kama baba na mtoto.
Alisema
miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na muda wa kurudi nyumbani katika mkataba
waliosaini wote waili (baba na mtoto) ambao ulisema mwisho wa kurudi nyumbani kwa
mtoto huyo ni saa nne kamili usiku na sio zaidi ya hapo.
Mara
baada ya kusaini mkataba huo ambao nakala yake ilipelekwa kituo cha polisi Bagamoyo
kama ushahidi, mtoto huyo kwa siku kadhaa alikuwa anakiuka yale waliyokubaliana
kwenye mkataba na hasa muda wa kurudi nyumbani na kwamba amekuwa akirudi
nyumbani zaidi ya saa nne kinyume na makubaliano na bila ya kutoa maelezo
yoyote yenye kuridhisha .
Kufuatia
hali hiyo tarehe 19 mwezi machi 2019, ambapo ni siku ya saba toka kusainiwa kwa
mkataba huo wa makubaliano, kijana huyo alirudi nyumbani saa tano na nusu usiku,
ambapo alikuta milango imefungwa hali iliyomlazimu kugonga ili afunguliwe.
Aidha,
mara baada ya kijana huyo kugonga mlango baba yake alisema "sikufungulii
mlango kwakuwa umekiuka mkataba wetu kuhusu muda wa kurudi nyumbani ambao
mwisho ni saa nne kamili usiku".
Kufuatia
majibu hayo ya baba yake, kijana huyo hakuweza kujitetea kwa kuongea chochote
na badala yake alichukua mawe na kuyapanga kwaajili ya mashambulizi ambapo
alipiga mlango kwa mara kadhaa na kusababisha majirani kutoka ili kushuhudia
kinachoendelea kutokana na kishindo kikubwa kilicholia hapo nyumbani.
Kijana
huyo aliendelea kushambulia mlango huo huku akisema kuwa "nitaingia ndani
kwa namna yoyote ile na kwamba wewe (baba) huna uwezo wa kunizuia"alisikika kijana huyo akimjibu baba yake.
Katika
harakati zake za kuvunja mlango alifanikiwa kuvunja kioo cha juu ya mlango na
kuingia ndani huku akiahidi kuendeleza mashambulizi kwa siku zinazofuata ikiwa
atawekewa masharti na kufuatwa fuatwa katika maisha yake.
Kesi
hiyo ya jinai Namba 120 ya mwaka 2019 iliyosikilizwa na hakimu Japheti Angilile
Masebo wa Mahakama ya mwanzo Mwambao mjini Bagamoyo ilihukumiwa siku hiyo hiyo baada
ushahidi kukamilika na mahakama kumtia hatiani mshitakiwa.
Akisoma
hukumu hiyo Hakimu Masebo alisema anamuhukumu mshitakiwa kwenda jela miezi sita
ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye tabia za kudharau wazazi wao na
kuvunja sheria za nchi.
Aliongeza
kwa kusema kuwa, mshitakiwa alifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 326
kifungu kidogo cha (1) sura ya 16 kanuni ya adhabu iliyorejewa mwaka 2002.
Awali
mshitakiwa alipotakiwa kujitetea alisema alilazimika kuvunja mlango ili aingie
ndani akalale baada ya baba yake kukataa kumfungulia huku ikizingatiwa kuwa,
hana sehemu nyingine ya kulala.
"Mheshimiwa
Hakimu, huyu mie ndio baba yangu na pale ndio nyumbani kwangu nilivunja mlango
ili nikalale kwakuwa sina sehemu nyingine ya kulala" alisema kijana huyo
mara baada ya kutiwa hatiani.
Hakimu
Masebo alimtaka ajitetee ni kwanini Mahakama isimpe adhabu mara baada ya kumtia
hatiani, mshitakiwa alijibu "hapo nimemaliza, mheshimiwa utaamua
wewe"
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi nje ya Mahakama, baba mzazi wa kijana huyo ambae
hakutaka jina lake litajwe alisema amechukua uamuzi wa kumpeleka mahakamani
mwanae, baada ya njia tofauti za kumrekebisha kitabia kushindikana.
"Nimetumia
njia nyingi kumrekebisha kijana wangu lakini imeshindikana, huenda hii ikawa
njia sahihi ya kujifunza nidhamu kwa kijana huyu" Alisema baba huyo huyo wa mshitakiwa.
Aliongeza kwa kusema kuwa ninao uwezo wa kutengeneza kioo pamoja na huo mlango wote lakini kilichonifanya nimpeleke mahakamani kutaka ajifunze utii wa sheria ikiwa ni pamoja na sheria za nchi za mungu na zile mnazokubaliana na wazazi wako pia ni sheria zinazopaswa kutiiwa.
"sio kwamba siwezi kutengeneza huo mlango, au sio kwamba simpendi mwanangu hapana, nimefanya hivyo baada ya njia nyingi za kumrekebisha kufeli nadhani hii ndio njia sahihi kwake, Alisema mzazi huyo.
No comments:
Post a Comment