Friday, April 5, 2019

KIKWETE APONGEZWA CHALINZE.

Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, akijenga ukuta wa madarasa  katika shule ya msingi Kibindu, iliyopo kata ya Kibindu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo hii ilikuwa mwezi Machi 2018
Picha kutoka Maktaba yetu.
.............................................


Na Shushu Joel,Chalinze.

WANANCHI wa kata za Kibindu na miono, wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wamempongeza mbunge wa jimbo la chalinze Ridhiwani Kikwete kwa jinsi anavyojitolea katika ufanikishaji wa miradi ya maendeleo kwenye Nyanja za Elimu,Afya na maji.


Pongezi hizo zimetolewa na diwani wa kata ya Miono Juma Mpwimbwi  wakati  alipokuwa akikagua bweni la wanafunzi wa kike na majengo mawili ya madarasa  ya shule za msingi unaoendelea katika kata hiyo.


Alisema kuwa awali maeneo hayo yalikuwa na changamoto kubwa ya uhaba wa  miundombinu ya elimu, hasa upungufu wa vyumba vya madarasa amabavyo kutokana na kuwepo kwa miaka mingi vimekuwa na nyufa kubwa hivyo kuhatarisha maisha ya wanafunzi na hata walimu.


Mpwimbwi aliongeza kuwa alimuomba mbunge wake Ridhiwani Kikwete waweze kuona namna jinsi wanavyoweza kupata wafadhili au hata kupitia mfuko wa jimbo ili kuwasaidia watoto waliokuwa wakisoma katika shule hiyo ili wasomee kwenye vyumba vilivyo na ubora kama ilivyo kwa wengine jimboni humo.


Kufuatia ombi hilo, Mpwimbwi alisema alifanikiwa kupata fedha kutoka kwa Mbunge huyo ili kuhakikisha wanafanikisha ujenzi huo wa vyumba vya madarsa na bweni la watoto wa kike ili kuwanusuru na vijana wasio na nia njema kwa watoto wa kike.


Naye Halma Iddi mkazi wa kata hiyo ametoa pongezi zake kwa mbunge huyo na kumtaka kuendelea kuwa na moyo huo katika kuwasaidia ili watoto waweze kupata elimu wakiwa katika mazingira mazuri kama ilivyo katika shule zingine.


Aliongeza kuwa awali wanafunzi hao walikuwa na changamoto kubwa ya kusomea katika mazingira magumu  kutokana na majengo yaliyo mengi kuwa na nyufa.


Aidha  aliendelea kusema kuwa, wanampongeza mbunge huyo kwa wepesi wa kushughulikia jambo lolote lile mara tu anapoambiwa na wananchi wake.


Akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG kwa njia ya simu mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ni majukumu yake kuhakikisha anaishawishi serikali ili kufanikisha miradi ya maendeleo kwa wananchi wake wa chalinze.


Alisema kuwa wakati anaomba ridhaa ya kuwatumikia aliwahakikishia kuwa yeye atakuwa ni mbunge wa maendeleo na sasa wananchi hao wanayaona wao wenyewe kwani awali tulikuwa na wakati mgumu lakini kwa sasa kila jambo linalohusu maendeleo katika jimbo la chalinze kila kitu kinaenda vizuri.


Hivyo Kikwete amewataka wananchi hao kuendelea kuilinda miradi hiyo ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu kwa kutumiwa na kizazi na kizazi cha chalinze.


Aidha alisema kuwa kuna miradi mingi inakuja chalinze hivyo wananchi wanatakiwa kuchangamkia fursa zitakazokuwa zinajitokeza kwa kuomba ajira katika viwanda, na kwamba kitu cha kujivunia malighafi zipo za kutosha chalinze na kuongeza kwa kusema kuwa, tunazidi kuwaomba wawekezaji wazidi kufika kwa wingi jimboni humo ili kuanzisha viwanda vya aina mbalimbali
 
MBUNGE wa jimbo la Chalinze,wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani  Kikwete (mwenye kofia ya CCM) akiwa katika jimbo lake kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment